Home Mchanganyiko TAMKO LA TUME KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA.

TAMKO LA TUME KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA.

0

*******************************

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na Watanzania wote katika
kuadhimisha Siku ya Mazingira duniani ambayo kilele chake ni Juni 5, 2020.

Kama Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Kitaifa Mwaka huu inavyosema Tuhifadhi Mazingira: Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, hivyo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nayo kupitia Maadhimisho haya inapenda kuwakumbusha Wananchi wajibu wao wa kutunza na kuhifadhi mazingira kwa sababu ustawi wa viumbe hai akiwemo binadamu unategemea mazingira mazuri.

 

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira yanatoa fursa kwetu sote kutafakari juu ya mazingira yetu
na kuweka mikakati mizuri ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

 

Haki ya Mazingira safi ni haki muhimu sana kwa amendeleo ya binaadamu. Uhifadhi wa haki
hii unaimarisha upatikanaji wa haki nyengine za binaadamu zikiwemo haki ya kuishi, haki ya
kumiliki mali, haki ya kupata chakula, makaazi, maji safi na salama. Vivyo hivyo, uchafuzi wa
mazingira unaathiri upatikanaji wa haki hizo.

 

Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora inatambua juhudi mbali mbali za kisera, kiutawala na kisheria ambazo serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa zikichukuwa kuhifadhi haki ya Mazingira.

 

Pamoja na jitihada hizo kumekuwa na changamoto mbali mbali ambazo zimekuwa zikiathiri uhifadhi wa haki ya mazingira.

 

Changamoto hizo ni pamoja na uelewa mdogo wa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, ukataji miti ovyo, ujenzi holela usiofuata mipango miji na utiririshaji
majitaka wakati mwingine maji yenye sumu kutoka viwandani kuelekea kwenye makaazi ya
watu.

 

Tume inaiomba serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira na Wizara inayohusika na mazingira Zanzibar kushirikisha wadau mbalimbali katika harakati za kuhamasisha jamii kutunza mazingira na kuwaelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira.

 

Tume pia inaziomba mamlaka zote zinazosimamia uhifadhi wa mazingira Tanzania kusimamia ipasavyo sera, sheria na miongozo yote inayoongoza katika uhifadhi wa mazingira ili kuepusha mabadiliko ya tabia nchi.

 

Tume inawashauri Watanzania kujiweka mbali na shughuli zinazochangia kusababisha uharibifu
wa mazingira nchini na inawaomba watoe taarifa kwa mamlaka husika pale wanapoona mtu,
kikundi cha watu, Kampuni ama taasisi yoyote ambayo inafanya shughuli zinazochangia
kuharibu mazingira.

 

Tume inapenda kukumbusha kuwa katika kuelekea maadhimisho haya wananchi wasisahau
kuendelea kuchukua tahadhari ya maradhi ya Korona ili kuyatokomeza kabisa maradhi hayo
ambayo kwa mujibu wa taarifa za mamlaka husika yamepungua kwa kiasi kikubwa.

 

Aidha, Tume inaipongeza Serikali kwa kuamua kuadhimisha Siku hii ya Mazingira kwa kutumia
vyombo vya habari ili kuepuka mikusanyiko kwa lengo la kuendelea kujikinga na maambukizi
ya Korona.