Mihogo ikiwa tayari kwaajili ya Chakula baada ya kuvunwa
Mboga Mboga
Mahindi mabichi baada ya kuvunwa
Mahindi makavu kwaajili ya kusaga na kutoa unga kwaajili ya Chakula.
*****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Tukiwa tunaelekea katika maadhimisho ya Siku ya Usalama wa Chakula Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Juni 7, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) siku hiyo litajikita kutoa elimu kwa jamii kuhusu Usalama wa Chakula.
Akizungumza katika Ofisi za Shirika hilo, Afisa Usalama wa Chakula TBS, Dkt.Analice Kamala amesema kuwa kila mtu yuko kwenye hatari ya kupata madhara ya kiafya. Hata hivyo makundi maalum kama vile wagonjwa, wajawazito, watoto na wazee wapo katika hatari zaidi ya kuathirika na chakula kisicho salama.
“Ikiwa mtu akitumia chakula ambacho si salama athari za kiafya huweza kujitokeza ndani ya muda mfupi (food poisoning) mfano; kuumwa tumbo, kutapika, kuhara na kuhara damu au baada ya muda mrefu mfano; kansa, upungufu wa kingamwili na udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano”. Amesema Dkt.Analice.
Dkt.Analice amesema kuwa pia athari za kiuchumi zinaweza kujitokeza ikiwa kuna chakula kisichosalama, athari hizo ni pamoja na kukataliwa kwa bidhaa za chakula zilizozidi viwango vinavyokubalika katika soko na
hivyo kukosa mapato,Kuongezeka kwa gharama za matibabu,Kupungua kwa nguvu kazi na uzalishaji mali na athari nyingine nyingi.
Aidha Dkt.Analice amesema kuwa ili kuwa na chakula salama, mfumo thabiti wa usimamizi na udhibiti wa uzalishaji, usindikaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula unahitajika.
“Lengo kuu la kuwa na mfumo imara wa chakula salama ni kujenga mazingira ambayo yatatoa uhakika wa uzalishaji chakula ambacho ni salama ili kulinda afya ya mlaji na kukuza biashara. Misingi imara ya usimamizi wa usalama inahusisha mambo yafuatayo; Uwepo wa sheria, Muundo wa kitaasisi (usimamizi), Mfumo wa ukaguzi na ufuatiliaji, Huduma za maabara na elimu kwa umma”.Amesisitiza Dkt.Analice.
Kauli mbiu ya mwaka huu kwenye Maadhimisho ya Siku ya Usalama wa Chakula Duniani 2020 ni “Usalama wa Chakula ni Jukumu la Kila Mmoja”.