Home Makala SAFARI YA MABADILIKO IMEANZA SASA, WASIOIMUDU WAJITAFAKARI

SAFARI YA MABADILIKO IMEANZA SASA, WASIOIMUDU WAJITAFAKARI

0
Na.Imani Mbaga,Dar es salaam
NANI anatamani kuufuata mshale wa saa unaorudi nyuma badala ya kusonga mbele? Swali langu kwa waungwana wale wanaowaza mawazo chanya tena wenye ndoto halisi za kuona ukuaji unaozingatia mabadiliko ya dhati, yenye kuleta manufaa kwa wanaopenda jambo fulani.
  Yanga, klabu kongwe kabisa nchini imeingia kwenye kumbukumbu za historia mpya ya klabu yao kwa kutia saini kuanza kwa MCHAKATO wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo, kutoka mfumo wa kizamani unaotoa mianya ya “upigaji” kuelekea mfumo wa kisasa unaotoa fursa ya maendeleo na faida.
  Tumejadili muda mrefu sana, kuhusu umuhimu wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa mpira wetu.
 Kulikuwa na ugumu sana wa kufikia muafaka wa jinsi gani vilabu vyetu vihame kutoka mfumo wa zamani kwenda kwenye mfumo wa kisasa.
  Hatua ambayo Yanga wameifikia ni hatua ya kupongezwa, kwakuwa hapo kabla hili suala lilikuwa haliwezi kuzungumzwa kwa amani bali kila wakati liliishia kwenye vurugu na kudidimiza maendeleo ya klabu.
  Kama leo Yanga wanakubali kwa pamoja kwamba wanahitaji mabadiliko, basi kitendo cha kuona na kukubali tu, kinapaswa kupongezwa wala si kuvunjwa moyo.
  Baada ya kukubaliana kwa pamoja, hatua inayofuata ni kujadili ni mabadiliko ya aina gani ambayo Yanga wanayahitaji, yafanyike kwa njia ipi, na baada ya hapo wapitie hatua zipi.
 Kwa mtu mwenye akili na anayependa maendeleo, anayewaza kufika mbali, anajua adui namba moja wa mipango ya maendeleo ni “kukurupuka”.
  Tunapozungumzia mabadiliko ni pamoja na madiliko ya namna tunavyofanya mambo yetu.
 Katika suala la kubadili mfumo, unahitaji ushauri wa kitaalamu, toka kwa wataalamu waliojaa weledi, ambao ubabaishaji siyo sehemu ya maisha yao, na hapa ndipo kampuni ya LA LIGA inapoingia.
 Mshauri “consultant” ni lazima awe na sifa kubwa tatu (kwa mtazamo wangu) ambazo ni
I) WELEDI (professionalism)
II) UZOEFU (experience)
III) UWEZO (competency)
  Kwangu mimi nikipata “mshauri mwelekezi” mwenye hizo sifa tatu hapo juu, ninaridhika na ninapata amani na kujiamini kwamba atakayenishauri ni “mtu sahihi” na kwamba atanipitisha kwenye njia sahihi.
 Hakuna aliyefanikiwa duniani kwa kuzitegemea akili zake mwenyewe bila ya kuchukua “uzoefu” wa mwingine katika jambo husika.
  Kuwapa Laliga jukumu la kuishauri Yanga njia ya kupita ili kufanikisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji sioni mahali pa kutilia shaka, kwa pande zote mbili.
 Katika hili palihitajika vitu vitatu vya muhimu
 Kwanza, nia ya dhati ya kubadilika kwa upande wa Yanga, hili linapatikana kwenye mioyo ya wana Yanga wenyewe.
 Pili, misuli ya kifedha ili kufadhili mchakato wa mabadiliko ambao ni wazi kwamba una gharama kubwa, hili unalipata kwenye mfuko wa GSM
 Tatu, unahitaji mtu mwenye utaalamu, uzoefu na ujuzi wa kukushauri njia sahihi utakayoipitia, hili tunalipata katika ubongo wa watu wa kampuni ya Laliga.
  Kwangu mimi huu ushirikiano “kolabo” ya (mioyo ya wana Yanga,mfuko wa GSM na ubongo wa Laliga) naamini matokeo yake yatakuwa Yanga bora ya karne ya 21, ambayo kupigania Uhuru itakuwa historia yake, uendeshaji utakuwa wa kisasa na mafanikio yatakuwa sifa yake, na mioyo ya wana Yanga itabaki na furaha ya kipekee.
 Shaka inaanzia wapi ikiwa miaka 85  isiyo na akaunti ya fedha benki wala ushiriki wa kudumu na mafanikio yanayoonekana katika michuano ya kimataifa, itoshe kutupa shaka dhidi ya mfumo wa “kizamani” wa uendeshaji wala siyo mchakato wa kuhama toka mfumo huo kuelekea kwenye mafanikio.
  Tukumbuke tu, mafanikio ni gharama, huwezi kuota kupata fedha bila kupoteza fedha kwanza hiyo ni dhambi kubwa katika uwekezaji wa aina yoyote.
 Tutoe nafasi kwa uongozi, mdhamini na mshauri kutuonyesha njia, tuwape ushirikiano “support” ya hali na mali ili tuweze hatimaye kuwa sehemu ya historia kubwa ya klabu yetu kongwe.
 Mlinzi wa kwanza wa mchakato huu, ni kila mpenda mabadiliko, wala tusiruhusu watu wachache wenye chuki na maslahi binafsi watuharibie   ndoto yetu ya miaka zaidi ya 20 ya safari ya mabadiliko
 Daima mbele…..💪