Mama mzazi wa Christopher Mfinanga akiweka shada la maua wakati wa mazishi yaliyofanyika jana Juni 3, 2020 katika makaburi ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mchungaji Bill Grahama Msangi wa KKKT Usharika wa Vuchama akihitimisha ibada ya mazishi ya aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga wakati wa mazishi yaliyofanyika jana Juni 3, 2020 katika makaburi ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Makaburi mawili, moja la Baba na jingine la mwana. Kulia mbele ni kaburi la aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga na la kushoto ni la Baba yake Mzee Edward Dologha Mfinanga aliyefariki jijini Arusha Mei 19, 2020 na kuzikwa Mei 21, 2020 kijijini kwake Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mama mzazi wa aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga akipita kuaga mwili wa mwanaye wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika jana Juni 3, 2020 kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Jeneza lenye mwili wa Christopher Mfinanga likiwa kaburini wakati wa mazishi yaliyofanyika jana Juni 3, 2020 katika makaburi ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Tom Apson akiweka udongo kwenye kaburi la aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga wakati wa mazishi yaliyofanyika jana Juni 3, 2020 katika makaburi ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Baba mdogo wa marehemu, Alhaj Mzee Yusuf Mfinanga akiweka udongo kwenye kaburi la aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga wakati wa mazishi yaliyofanyika jana Juni 3, 2020 katika makaburi ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mchungaji Bill Grahama Msangi wa KKKT Usharika wa Vuchama akihitimisha ibada ya mazishi ya aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Christopher Mfinanga wakati wa mazishi yaliyofanyika jana Juni 3, 2020 katika makaburi ya familia kijijini Mangio, Vuchama, wilayani Mwanga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
***********************************
MKUU wa Wilaya ya Mwanga, Bw. Tom Apson ameongoza mazishi ya aliyekuwa Mpigapicha wa Waziri Mkuu, Bw. Chris Mfinanga yaliyofanyika kwenya kijiji cha Mangio, Vuchama, wilayani humo.
Akizungumza na waombolezaji kijijini hapo jana (Jumatano, Juni 3, 2020), Mkuu huyo wa Wilaya ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bibi Anna Mgwira alisema Chris Mfinanga alikuwa mtu aliyejaa upendo ndiyo maana wengi wanahuzunishwa na kifo chake.
“Chris alikuwa mtu mcheshi na mwenye upendo, alisaidia wengi lakini tusisahau kwamba Mungu ndiye mtoa riziki. Msikate tamaa kwa sababu Mungu yupo na alimwezesha Chris na ndiyo maana aliweza kuwasaidia wengine na hata kuwasomesha watoto wenu.”
“Ninawasihi muamini kuwa Yesu yupo na kwake kuna faraja. Amini Yesu yupo na usiamini katika mganga wa kienyeji au ushirikina. Tuache ramli, tumtegemee Mungu nasi tutapata faraja,” alisisitiza.
Mapema, akiongoza ibada hiyo, Mchungaji Kiongozi wa KKKT Usharika wa Vuchama, Bill Graham Msangi aliwataka waombolezaji waweke mambo yao sawa na Mungu wao pamoja na majirani wanaoishi nao.
Akitoa mahubiri kutoka kitabu cha Ufunuo wa Yohana (14:13), Mchungaji Msangi alisema watu wanaomwamini Kristo wana heri kwa sababu wanapoaga dunia ni sawa na watu wanaoenda kupumzika baada ya taabu zao hapa duniani. “Wanaokufa katika Bwana wanaenda kupumzika baada ya taabu zao. Wana heri sababu matendo yao yanafuatana nao.”
“Kama wewe ni mchawi au mpiga ramli na kazi yako ni kuchonganisha watu, au wewe ni kibaka au mfitini, je hayo matendo yako utaenda nayo wapi? Kule kwenye pumziko siyo kwao watu wa aina hiyo,” alisema.
“Neno la Mungu limesema; bali wao wasioamini, waongo wote, wachukiao na wezi wote na waabuduo sanamu, sehemu yao ni kwenye ziwa la moto ambao hata mende hawaungui. Hata uwe tajiri kiasi gani, au uwe mzuri kiasi gani au uwe baunsa, hautaweza kuzuia kuingia kwenye jehanamu ya moto eti kwa sababu ya ubaunsa wako.”
“Tunapaswa tujiandae kwa sababu siku ikifika, Mungu haatangalia uzuri ulionao. Yeye Mungu ni mzuri kuliko huo uzuri wako. Shetani alikuwa mzuri sana lakini alipoasi alifukuzwa.”
Aliwasihi wafiwa na wakazi wa kijiji hicho hao wawe na umoja ili amani iweze kutawala. “Umoja ukae miongoni mwa familia, ukae miongoni mwa kaya nyingine na wanavijiji wote. Tukiishi kwa namna hiyo, amani itatawala kwa sehemu kubwa.”
Naye Padre Japhet Njaule wa Parokia ya Vuchama ambaye aliongoza mazishi ya Baba yake Chris Mei 21, 2020, aliwataka waombolezaji wamtumaini Mungu na waishi kwa kujiandaa na kuwa tayari wakati wote.
“Sisi sote ni mali ya Bwana. Tuishi leo na sasa kana kwamba ni saa hii tunaondoka na wala tusiwaze kuhusu kesho yetu. Tukumbuke kuwa Mungu ana mpango na maisha ya kila mmoja wetu,” alisisitiza.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Fadhili Liwaka aliwataka wanafamilia wapate faraja kutoka kwa Mung una wala wasiumizwe na msiba wa Chris. “Tusione ajabu ya msiba huu kwa sababu hili ni jaribu la moto na Mungu anatukumbusha juu ya kuzaliwa, kuishi na kufa. Hakuna binadamu ambaye anaweza kukwepa kifo na hakuna mahali mapenzi ya mwanadamu yanaweza kuzuia kifo cha yule unayempenda.”
Alisema: “Msiba unapotokea, unatukumbusha kuwa tutarejea kwa Mungu, pia utakuja kutuunganisha kama ndugu na kutujulisha kuwa hii neema ya Mungu na si jambo la kibinadamu na tatu unatukumbusha juu ya kujenga, amani, utulivu na kukubaliana na matokeo.”
Naye Baba mdogo wa marehemu, Alhaj Mzee Yusufu Mfinanga aliwashukuru madaktari na wauguzi waliomhudumia Christopher wakati akipatiwa matibabu. Pia aliwashukuru ndugu, jamaa, marafiki, majirani na wafanyakazi wenzake kwa ushirikiano mkubwa waliounesha. “Ushirikiano huo ni dalili tosha kwamba Christopher alikuwa akiishi vizuri na watu.”