Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange KIhongole katikati akiwa na Mashono Said Amir wa pili kushoto ambaye alipatwa na ugonjwa wa kifua kikuu sugu na kukimbilia shambani ili asifahamike na wataalam wa Afya akiwa na wake zake Lios Bakari kushoto na Sharifa Maneno wa pili kulia mara baada ya kurudi kutoka katika matibabu Hospitali ya Kigong’oto mkoani Kilimanjaro ambapo ndiyo Hospitali inayohudumia wagonjwa wa kifua kikuu sugu,wa kwanza kulia ni mfanyakazi wa kitengo cha kifua kikuu Hospitali ya wilaya Tunduru Editha Buberwa.
Picha na Mpiga Picha wetu
………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
HOSPITALI ya wilaya Tunduru kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma,imeanza kampeni ya kuwafuatilia watu waliobainika kupata ugonjwa wa kifua kikuu na kuanzishiwa dawa ili kuhakikisha wanakuwa na ufuasi mzuri wa matumizi ya dawa kadri ya maelekezo waliyopewa na wataalam.
Kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa wilaya ya Tunduru kuungana na wizara ya Afya hapa nchini na Shirika la Afya Dunia(WHO) ya kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu ifikapo mwaka 2030.
Hivi karibuni wilaya ya Tunduru ilizindua kampeni ya uelimishaji, uchunguzi na upimaji wa kifua kikuu ijulikanayo kama kilinge kwa kilinge, nyumba kwa nyumba na shule kwa shule ambayo inakusudia kuwafikia wananchi wote katika wilaya hiyo.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole amesema, katika kampeni hiyo wataalam wa kitengo cha kifua kikuu watamfikia kila mgonjwa aliyebainika kuwa na TB na kuanzishiwa dawa wakiwemo waliobainika kuwa na kifua kikuu sugu.
Alisema, wale watakao bainika kukatisha kunywa dawa wataendelea kupewa elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya dawa za kifua kikuu pamoja na madhara yanayoweza kupatikana kwa mgonjwa kupuuzia matumizi yake.
Kihongole alisema, mkakati mwingine kwa ambao wamekatisha dawa ni kuwashirikisha viongozi wa serikali ya eneo waliopo ili kuwafuatilia katika matumizi ya dawa wakishirikiana na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Kwa mujibu wa Kihongole,Hospitali ya wilaya ya Tunduru imepewa lengo la kuwaibua wagonjwa 647 katika mwaka 2020 ambapo kila robo mwaka inatakiwa kupata wagonjwa 161, hata hivyo katika robo ya kwanza ya Januari- Machi wamepata wagonjwa 180 sawa na asilimia 111 na wamevuka lengo walilopewa.
Alisema, katika robo ya pili ya Aprili- Juni,hadi kufikia Mei 30 tayari wamepata wagonjwa 102 na wanaamini kupitia kampeni hiyo na mapambano wanayoendelea watafanikiwa kuvuka lengo walilopewa la kupata wagonjwa 161 kwa kila robo.
Alisema, hii inaonesha tofauti kubwa kati ya mwaka 2019 na 2020 kwa sababu robo ya kwanza 2019 walipata wagonjwa 130 sawa na asilimia 85.6 lakini robo ya Januari-Machi 2020 wamepata wagonjwa 180.
Alisema, kadri kampeni hiyo inavyoendelea ndipo idadi ya watu wenye maradhi ya ugonjwa wa kifua kikuu nayo inaongezeka ambapo ameitaka jamii kushiriki katika kampeni ya kuibua watu wenye maradhi ya kifua kikuu katika maeneo yao.
Mmoja wa wagonjwa wa kifua kikuu mkazi wa kijiji cha Nakapanya kata Nakapanya ambaye alipata ugonjwa wa kifua kikuu sugu na kisha kukimbilia shambani ili asiendelee kutumia dawa,ameitaka jamii kutopuuza ugonjwa huo na kuhakikisha wanapata matibabu haraka pindi wanapobainika kupata ugonjwa huo.
Mashono ambaye ana familia ya wake wawili na watoto wanane alisema, alipata maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu mwishoni mwa mwaka jana,lakini alichukua uamuzi wa kukimbilia shambani ili asijulikane hadi kitengo cha kifua kikuu Hospitali ya wilaya Tunduru ilipomuibua na kumuanzishia dawa kwa lazima.
Ameishukuru Serikali kwa jitihada kubwa iliyofanya ya kuokoa maisha yake,kwa kumpeleka Hospitali ya Kibong’oto kwa ajili ya kupata matibabu ya ugonjwa wa kifua kikuu sugu ambapo sasa afya yake imeimarika licha ya kutakiwa kuendelea kunywa dawa hadi mwaka 2021.
Aidha,ameipongeza Hospitali ya wilaya Tunduru kupitia wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma kwa kufanya kampeni mbalimbali za kuelimisha jamii, uchunguzi na kuwaanzishia tiba watu wanaobainika kupata ugonjwa huo kwani imesaidia sana kuokoa maisha ya wananchi wengi.
Ameiomba Serikali kupitia wizara ya afya kuongeza bajeti ya fedha,dawa na kuajiri wataalam wa Tb, ili waweze kufanya kazi ya kuokoa maisha ya wananchi hasa wale wanaoishi maeneo ya vijijini pamoja na wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na kuwafuatilia wagonjwa wote waliobainika kupata maradhi hayo ili waendelea kunywa dawa.
Alisema, ugonjwa wa kifua kikuu una mateso makubwa kuliko ukimwi,na iwapo mgonjwa atafanya uzembe katika matumizi ya dawa ni rahisi kupoteza maisha na kuwaasa wale walioibuliwa kupitia kampeni zinazofanywa na kitengo cha kifua kikuu kuzingatia matumizi ya dawa kwa usalama wa maisha yao