*******************************
NA MWAMVUA MWINYI,CHALINZE
MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Zaynabu Kawawa, ameikabidhi Halmashauri ya Chalinze ,vitambulisho vya Mjasiriamali vipatavyo 10,106 na kuagiza wasibughudhiwe.
Aidha amewaonya Watendaji wataokwamisha zoezi la usambazaji wa vitambulisho maalumu kwa ajili ya wajasiriamali.
Katika hafla fupi ya makabidhiano hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya Sekondari Lugoba, Kawawa alisema, vitambulisho hivyo vilivyotolewa na Rais John Magufuli kwa wajasiriamali wadogo, vinalenga kuwaondolea adha walengwa hao ambapo kupitia mpango huo Serikali kupitia Mamlaka ya kukusanya Mapato TRA itakuwa imekusanya pesa za kutosha.
Akizungumza kabla ya kukabidhi vitambulisho hivyo, Kawawa alibainisha,kwa mwaka huu wilaya hiyo yenye Halmashauri mbili ya Chalinze zimepata vitambulisho 17,000 ikiwemo Chalinze wamepata zaidi ya 10,106 na Bagamoyo ni 6,891.
Hata hivyo,alisema hatokuwa na msamaha kwa atayeonekana kuwa kikwazo kwenye zoezi hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,Zaynabu Makwinya alieleza, wamejiandaa kuhahakisha zoezi litamwenda vizuri.
Alisema, wamejipanga vizuri kuhakikisha kwamba vitambulisho hivyo vinauzwa na hadi Juni 5 vitakuwa vimemalizika, huku akieleza kuwa kuna gari maalumu linalotumika kwa ajili ya zoezi hilo.
“Kwa Watendaji ambao watamaliza mapema vitambulisho vyao watawasiliana na Maofisa Tarafa, ili tujulishwe tumwambie ofisa Ushirika awapelekee waendelee na zoezi la uuzwaji wa vitambulisho hivyo,” alisema Makwinya.
Kaimu Ofisa Mfawidhi wa TRA Kanda ya Chalinze David Tawa alieleza ,zoezi hilo ni muhimu kwakuwa wajasiriamali wanaingia katika mfumo wakutambulika.