MKUU wa Mkua wa Tanga Martine Shigella akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo leo ambao hawapo pichani kuhusu ziara maalumu ya
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa itakayoanza kesho Jumatatu
*************************************
WAZIRI mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwasili jijini Tanga kesho June Mosi Mwaka huu kwa ziara maalum ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa agizo lake kwa bodi ya Mkonge alilolitoa mapema mwezi machi mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo mkuu wa mkoa wa Tanga Martin Shigela alisema waziri mkuu anatarajiwa kuzindua Jengo la Bodi ya Mkonge lililopo Jijini Tanga na baadae atatembelea Taasisi ya utafiti ya Mlingano na kukagua vitalu vya zao hilo.
Shigela alisema kuwa ziara hiyo ni mahususi kwa ajili ya kufuatilia maagizo aliyoyatoa machi 1, mwaka huu baada ya kupokea taarifa ya kamati maalum aliyounda kwa ajili ya ufuatiliaji wa mali za bodi ya mkonge.
“Baada ya taarifa hiyo yapo maelekezo aliyoyatoa, hivyo ziara yake hii ni mahususi kwa ajili ya kuja kuona maagizo aliyoyatoa ya ufuatiliaji wa kufufua zao la mkonge na namna ya utekelezaji wa urejeshwaji wa mali ambazo zilitajwa kuwa zilizoporwa kinyume cha utaratibu na sheria” alifafanua.
Aidha Shigela aliwashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari mkoani humo kwa namna walivyowajibika na kushirikiana katika nyanja mbalimbali kufanikisha utoaji wa taarifa kwa wananchi kwa urahisi na wakati.
“Niwashukuru sana ninyi waandishi wa habari kwa namna mlivyowajibika katika ile ziara ya waziri mkuu pamoja na kupigania kwa pamoja mapambano dhidi ya corona na kuwatetea wananchi wetu hasa katika eneo la mpakani kule horohoro” alieleza.
Hata hivyo Shigela aliwataka waandishi wa habari kushiriki kikamilifu katika ziara hiyo ya siku moja kwani ziara hiyo inalenga kuleta manufaa kwa mkoa wa Tanga kupitia zao la mkonge kutokana na kwamba ndio zao kubwa linalotegemewa kibiashara.
Alibainisha kwamba ujio wa Waziri Mkuu Majaliwa ni ukombozi kwa mkoa wa Tanga kwani endapo zao la mkonge litafufuliwa na kuimarika mkoani humo wananchi wataweza kujikwamua kiuchumi kutokana na kilimo cha zao.
“Ziara hii kwetu sisi ni ukombozi mkubwa kwasababu zao la mkonge kwa mkoa wa Tanga ndio zao mahususi na ndio zao kuu tunalolitegemea katika mazao ya biashara, na tuna uhakika tukifufua zao letu la mkonge tutakuwa na uhakika wa wananchi wa wananchi wetu kujikwamua katika umasikini” alisema.