Home Michezo LIGI ZOTE KUPIGWA NYUMBANI NA UGENINI MASHABIKI NAO DIMBANI

LIGI ZOTE KUPIGWA NYUMBANI NA UGENINI MASHABIKI NAO DIMBANI

0

********************************

Na.Alex Sonna 

Serikali imeweka wazi kuwa ligi zote zitachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini bila kuwepo vituo kama ambavyo awali ilielekezwa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas leo Jijini Dar es salaam .

Dr. Abass amesema kuwa suala hilo limezingatia maoni ya Wizara ya Afya pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya michezo.

“Serikali imeridhia mfumo wa michezo ya soka uchezwe kama ilivyokuwa ukifanyika awali, yaani kwa mfumo wa nyumbani na ugenini, kabla ya Virusi vya Corona.

“Awali ilipangwa ichezwa kwa vituo na ilitokana na kuwepo kwa Virusi vya Corona lakini kwa kuwa hali inazidi kuwa shwari na Serikali imeridhia kuwe na mechi za nyumbani na ugenini kwa kila mechi ili kutoa burudani na furaha iendelee vilevile”, amesema Dkt.Abbas.

Dkt.Abbas amesisitiza kuwa Jambo la msingi ni kuona kwamba utaratibu unafuatwa ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona kwani licha ya kwamba hali imekuwa shwari lakini ni lazima kuchukua tahadhari.

“Naliagiza Baraza la Michezo la Taifa kwa kuzingatia Mwongozo wa afya Michezoni, kuratibu utekelezaji wa maelekezo haya kwa kufanya tathmini na kutoa maelekezo mahsusi juu ya namna ya urejeshaji wa michezo mbalimbali nchini”, ameelekeza Dkt. Abbasi

Vituo ambavyo vilipangwa awali ilikuwa ni kwa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho kituo cha Dar es Salaam na zile za Ligi Daraja la Kwanza na la Pili zingechezwa Mwanza.

Hii ilikuwa ni kutokana na kuchukua tahadhari dhidi ya janga la Virusi vya Corona ambalo linaivuruga dunia.

Ligi inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 13 huku ratiba ikitarajiwa kutolewa leo, Mei 31.

Aidha Serikali imetoa mwongozo wa kufuata katika michezo ya Ligi Kuu za Soka Nchini ambazo zinatarajiwa kuanza Juni Mosi, 2020, hivyo ni muhimu kuzingatia na kwa yoyote atakayekiuka taratibu hizo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake – Dkt. Hassan Abbas