Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki
Shemdoe wa kwanza (kulia) akizungumza na Mkurugenzi
Kiwanda kuzalisha mafuta ya kupikia cha Bugili Investment Bw. Nkuba Bugili wa kwanza (kushoto) alipofanya ziara katika kiwanda hicho kilichopo Wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu. {Picha na Wizara ya Viwanda na Biashara}
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki
Shemdoe wa kwanza (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa
kiwanda cha Bugiri Investment Bw.Nkuba Bugiri alipokuwa
anamueleza mambo mbalimbali kuhusu kiwanda hicho. Wa
kwanza (kushoto) ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda
na Biashara Bw. Ludovick Nduhiye.
Sehemu ya mashine za kukamulia mafuta ya alizeti katika
kiwanda cha Bugiri Investment kilichopo Wilaya ya Maswa
Mkoa wa Shinyanga.
Sehemu ya shehena ya mbegu za alizeti zilizopo kiwandani
hapo zikiwa tayari kwa ajili ya uzalishaji.
*********************************
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amewataka Watanzania kuwekeza katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za ndani.
Prof. Shemdoe aliyasema hayo Mkoani Simiyu alipokuwa katika ziara ya siku moja kutembelea Viwanda katika Mkoa huo.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu na ujumbe wake walipata fursa ya kutembelea kiwanda kipya cha kuzalisha mafuta
ya alizeti cha cha Bugari Investment Ltd kinachomilikiwa na Mtanzania kwa asilimia 100.
Prof Shemdoe alisema Bw. Bugari ameonyesha umuhimu wa kuwa na malengo katika kutekeleza jambo lolote.
“ukiwa na malengo unaweza kufanya kitu chochote, hivyo natoa rai kwa watanzania wengine ambao wanaweza kuiga mfano huu kufika mahali hapa na kujifunza, maana yote yanawezekana ukiweka nia”.
Kiwanda cha Bugari Investment Ltd kimejengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 2 kinatarajiwa kutoa ajira kwa Watanzania 65 ikiwa ni ajira za kudumu na za muda pamoja na kuchangia mapato kwa Serikali kupitia kodi mbalimbali.
Prof Shemdoe aliishukuru Serikali ya Mkoa kwa kumpa ushirikiano mwekezaji huyo na kumuwezesha kufanikisha kutimiza azma yake ya kujenga kiwanda.
Pia alizishukuru Taasisi za fedha kwa kumuamini na kumpatia mkopo uliofanikisha kujenga kiwanda hicho.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Bw. Festo Kiswaga alisema wananchi wa Simiyu na mikoa ya jirani wamepata uhakika wa soko la alizeti kwa kuwepo kiwanda hicho.
“Tumekuwa tukiwasisitiza wananchi kulima, lakini changamoto ilikuwa upatikanaji wa masoko, hivyo uwepo wa kiwanda hiki utakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Mkoa huu na mikoa jirani’’.
Aidha alitoa wito kwa wananchi wa bariadi kuendelea kuzalisha alizeti kwa wingi ili kiwanda kiendelee kupata malighafi ya kutosha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Nkuba Bugari alisema ujenzi wa kiwanda hicho umeanza mwaka 2015 na upo katika hatua za mwisho na ujenzi na kinatarajiwa kukamilika na kuanza uzalishaji mapema hivi karibuni.
Bugari alisema wazo la kujenga kiwanda hicho alipata baada ya kupata hamasa kutoka kwa Mhe. Rais Dkt. John Joseph Magufuli alipotoa rai kwa Watanzania kujenga viwanda.
“Ndugu Watanzania wezangu tusiache bahati hii ya kuwa na Mhe. Magufuli, ni kwa namna gani Mhe. Rais anajitoa kwa ajili watanzania katika kufanikisha Tanzania ya Viwanda”.
Anasema mashine zilizofungwa katika kiwanda hicho zina uwezo wa kuchakata mbegu za alizeti, pamba na karanga.
Aliongeza kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata tani elfu arobaini na nane za mbegu za alizeti. Hivyo lengo lao ni kushika soko la ndani pamoja kuuza mafuta hayo nje ya nchi ya Tanzania.
Aidha aliwasisitiza watanzania kuwa na uthubutu
katika kutimiza malengo mbalimbali.