Muonekano wa Chelezo (kulia) ambacho kimekamilika kwa asilimia mia moja na maendeleo ya Ujenzi wa Meli Mpya ya MV Mwanza (kushoto) ambayo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 30 katika bandari ya Mwanza South, Mkoani Mwanza
Mafundi wa Kampuni ya Gas Entec kutoka Korea ya Kusini, wakiendelea na kazi ya ujenzi wa meli Mpya ya MV Mwanza katika bandari ya Mwanza South. Meli hiyo inatarajiwa kukamilika mapema mwaka 2021.
Mafundi wa Kampuni ya Kampuni ya Songoro Marine Limited, wakikamilisha kazi ya upakaji rangi kwenye meli ya MV. Butiama, katika bandari ya Mwanza South. Ukarabati wa meli umefikia asilimia 99.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Bandari ya Mwanza, Bw. Michael Palangyo,alipokagua maendeleo ya ukarabati wa jengo la abiria katika bandari ya Mwanza North, mwishoni mwa wiki.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, akikagua maendeleo ya ukarabati wa jengo la abiria katika bandari ya Mwanza North, mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli. Bw. Eric Hamis.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto), akimsikiliza Meneja Mradi wa meli mpya ya MV Mwanza, Mhandisi Vitus Mapunda, wakati akimweleza namna ya ukataji wa vyuma wakati Naibu Waziri huyo alipokagua maelekezo ya ujenzi wa meli hiyo, mwishoni mwa wiki.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
………………………………………………………………………………
Serikali imesema Meli ya MV Butiama, MV Viktoria na Chelezo zitakabidhiwa wakati wowote kuanzia sasa baada ya ukarabati mkubwa uliofanyika kukamlika kwa asilimia mia moja.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi Meli mpya ya MV Mwanza Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kufunguliwa kwa anga la Tanzania kutaruhusu wataalam kutoka nje kuwasili na kufanya ukaguzi wa mwisho kabla ya kuanza kutumia meli hizo na chelezo.
“Tungekuwa tushaanza kuzitumia meli hizi kwani ukarabati wake umekamilika kwa asilimia 99, ni imani yangu kuwa wataalam wanaosubiriwa watawasili siku chache zijazo na kukamilisha kile kilichobaki ili wananchi waanze kutumia usafiri huu’ amesisitiza Naibu Waziri Mhandisi Nditiye
Naibu Mhandisi Nditiye amesema pamoja na miradi hiyo Mradi wa Meli mpya ya MV Mwanza ujenzi wake unaendelea kwa kasi na unatarajiwa kukamilika mapema mwaka 2021.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli, Eric Hamis ameishukuru Serikali kwa kukamilisha malipo yote Mradi wa Ukarabati wa meli hizo pamoja na chelezo na kuahidi kuendelea kuisimamia kwa karibu ujenzi wa meli mpya unaoendelea.
Naye Meneja Mradi wa Meli mpya ya MV Mwanza, Mhandisi Vitus Mapunda amesema mradi wa meli hiyo unaendelea vizuri na kazi zinazoendelea kwa sasa ni kukamilisha tabaka la chini la meli hiyo kabla ya kuiweka kwenye chelezo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mhandisi Nditiye amekagua maendeleo ya ukarabati wa jengo la abiria katika bandari ya Mwanza North na kutoa wiki moja na nusu ukarabati huo kukamilika.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Mwanza, Michael Palangyo amemthibitishia Naibu Waziri Mhandisi Nditiye kuwa mradi huo wa ukarabati utakamilika kwa wakati na viwango ili kuweza kutoa huduma bora wakati meli za MV Butiama na Mv Viktoria zitakapoanza kutoa huduma kwa wakati wa Mwanza, mikoa ya jirani na visiwa vinavyozunguka mkoa huo.