Home Mchanganyiko KANYASU AITAKA TANAPA KUONGEZA IDADI YA MABANGO YA TAHADHARI BARABARANI KUPUNGUZA IDADI...

KANYASU AITAKA TANAPA KUONGEZA IDADI YA MABANGO YA TAHADHARI BARABARANI KUPUNGUZA IDADI YA WANYAMAPORI WANAOGONGWA

0
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Constantine Kanyasu akizungumza katika mkutano uliowakutanisha kwa pamoja Wadau wa Uhifadhi kujadili jinsi ya kulinda shoroba ya Kwakuchinja pamoja na maeneo mengine muhimu ya Wanyamapori  katika  ikolojia ya Tarangire na  Manyara katika mkutano uliofanyika katika wilaya ya Babati mkoani Manyara. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Babati, Mhe.Elizabeth Kitundu na kushoto ni Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dkt.Maurus Msuha.
Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya  Maliasili na Utalii, Lucy Saleko akitoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu utekelezaji wa  mkakati  wa kulinda shoroba na maeneo mengine muhimu ya Wanyamapori katika Ikolojia ya Tarangire na Manyara katika mkutano  uliofanyika katika wilaya ya  Babati.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akiwa kwenye picha ya pamoja  na baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge iliyopo pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
Mkurugenzi wa Utafiti wa TAWIRI, Dkt.Julius Keyyu akichangia hoja katika mkutano wa Wadau wa Uhifadhi uliolenga kujadili jinsi ya kulinda shoroba na maeneo mengine muhimu katika ikolojia ya Tarangire na Manyara.
Baadhi ya Wadau wa Uhifadhi walioshiriki katika mkutano huo uliofanyika katika wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Naibu Waziri wa Maliasili na IUtalii, Mhe. Constantine Kanyasu akisisitiza jambo katika  mkutano wa wadau wa Uhifadhi wa kijadili namna ya kulinda shoroba uliofanyika  katika wilaya ya Babati mkoani Manyara.
…………………………………………………………………………………….
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mhe. Constantine  Kanyasu ametoa agizo kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuongeza idadi ya mabango ya barabarani  yanayoonyesha tahadhari na  faini kwa madereva watakaogonga wanyamapori katika barabara ya Babati kuelekea Arusha.
Ametoa agizo hilo katika wilaya ya  Babati mkoani Manyara katika mkutano wa Wadau wa Uhifadhi uliowakutanisha Wataalamu mbalimbali kujadili namna ya kulinda mapito asili ya wanyamapori    (shoroba) pamoja na maeneo mengine muhimu ya wanyamapori ambayo yapo hatarini kutoweka kufuatia kushamiri kwa shughuli za kibinadamu
Mhe.Kanyasu amesema kukosekana kwa tahadhari hizo kunatishia kuharibika kwa ikolojia ya Tarangire na Manyara kutokana na idadi kubwa ya wanyamapori kuuawa kwa kugongwa na magari kila siku.
  Kwa mujibu wa takwimu jumla ya wanyamapori 588 wakiwemo simba na twiga waliuawa mwaka jana kwa kugongwa na magari yanayopita kwa spidi katika barabara hiyo
Kufuatia hali hiyo,  Mhe.Kanyasu ameitaka TANAPA kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanyamapori ya Burunge kukutana na Uongozi waTANROAD ili waweze kutekeleza agizo hilo la uongezaji mabango katika barabara hiyo.  
Akizungumzia mazimio ya Mkutano huo, Mhe. Kanyasu amemuagiza  Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuunda kikosi kazi cha wataalamu mbalimbali kwa ushirikiano wa ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Babati kutambua mipaka ya shoroba katika   vijiji
Mbali na maazimio hayo, Mhe, Kanyasu amemtaka Mkuu wa wilaya ya Babati  Kuhakikisha maeneo ambayo tayari yanatambulika kuwa ni shoroba yalindwe ili yasiendelee kuvamiwa.

Aidha, Mhe.Kanyasu amemtaka Mkuu wa wilaya ya Babati kuhakikisha anatoa maagizo kwa  Uongozi wa  vijiji vinavyozunguka shoroba hawagawi maeneo ambayo ni  shoroba  kwa  Wananchi kwa ajili ya shughuli za kibinadamu ikiwemo ujenzi na kilimo.
Mbali na kuweka mabango Mhe.Kanyasu amesema kuna haja ya kuweka kamera barabarani ili kupunguza vifo vya wanyamapori wanaouawa kwa kugongwa na magari yanayopita mwendokasi katika barabara ya Babati kuelekea Arusha.
Akitaja athari za kuziba shoroba hizo,Mhe.Kanyasu amesema hali hiyo ikiendelea hivyo  Hifadhi ya Taifa ya Tarangire itakuwa  kisiwa na hivyo kuwafanya wanyamapori wakiwemo tembo ambao husafiri kwenda kuzaliana na ukoo mwingine wataanza kuzaliana ndugu kwa ndugu na hivyo kusababisha athari kubwa kijenetiki.
Kwa upande Mkuu wa wilaya hiyo, Elizabeth Kitundu amesema wananchi waliopo katika maeneo ya Shoroba wamekuwa wakitambua umuhimu wa maeneo hayo na wamekuwa wakitoa ushirikiano kwetu
Kutokanana hali hiyo, ” Ninakuahidi kupitia maafisa Ustawi wa Jamii tutendelea kutoa elimu kwa wanavijiji wanaoendesha shughuli za kibinadamu katika maeneo ya shoroba wafahamu kuwa ni hatari kwao na hivyo maeneo hayo yaachwe kwa ajili ya wanyamapori huku mchakato wa kisheria ukiendelea kutekelezwa.