*******************************
Na. Majid Abdulkarimu
Wakurugenzi wa Halmashauri nchini wametakiwa kuandaa miundombinu rafiki katika shule ili kuhakikisha wanaendelea kuchukua tahadhari za kuwakinga wanafunzi na maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Gerald Mweli jijini Dodoma baada ya kutembelea shule za sekondari za serikali na binafasi ili kuangalia maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha sita watakao rejea shule mosi Juni Mwaka huu.
Akizungumza Mweli amesema kuwa watendaji hao wahakikishe maeneo ya shule yanasambazwa vituo vya kunawa mikono na maji tiririka ili kuendeleza vita dhidi ya janga la Corona.
Mweli ameeleza kuwa wazazi na walezi wasiwe na hofu kwa wanafunzi kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wanakuwa salama wakiwa mazingira ya shuleni kwa kila shule kuwa na mhudumu wa afya karibu kwa ajili ya kutatua changamoto za kiafya zitakazo jitokeza katika maeneo ya shule.
Aidha Mweli amewaelekeza watendaji hao kusimamia kwa karibu na kuhakikisha shule zinachukua tahadhari za ziada katika kuwakinga wanafunzi kwa kufuata mwongozo wa wizara ya afya wa kupambana na ugonjwa huo.
“wakuu wa shule kuhakikisheni mnawajenga wanafunzi kisaikolojia na kuwaondolea hofu ili waweze kuzingatia masomo na akili yao kuweza kurudi katika hali ya kawaida”, amesisitiza Mweli.
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma(RAS), Maduka Kessy ameeleza mpango mkakati wa mkoa ulivyojipanga kuwapokea wageni na kuhakikisha Dodoma inakuwa salama na hakuna maambukizi mapya yanayojitokeza.
“ Mpaka sasa Dodoma inawagonjwa wawili ambao muda wowote wataruhusiwa kwasababu wanaendelea vizuri na hivyo tunataka kuhakikisha hatupati maambukizi mapya,”ameweka bayana Kessy.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Dodoma, Amani Mfaume amesema kuwa uongozi wake umechukua tahatahadhari zote zilizotolewa na wizara ya afya na kusisitiza kuwa watatumia wiki moja kukamilisha silabasi kwa masomo ya kemia na fizikia na kuwa wiki tatu kabla ya mtihani zitatumia kufanya marejeo ya masomo.
Huku naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Msalato, Neema Maro almeeleza shule yake ilivyojipanga kuwapokea wanafunzi wa kidato cha sita kwa kuweka vifaa, sabuni na vitakasa mikono kwa ajili ya kusafisha mikono katika kila bweni wakati wa kuingia madarasani na eneo la wazi.
Mwalimu Maro ameongezea kuwa kuwa wanafunzi watakapoingia tu, watapatiwa elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa huu na pia wameanza kushona barakoa ambazo watawagawia wanafunzi bure mara tu watakapofika shuleni.