Home Biashara MICHE BORA MILIONI 1.8 YA MICHIKICHI KUGAIWA BURE KIGOMA

MICHE BORA MILIONI 1.8 YA MICHIKICHI KUGAIWA BURE KIGOMA

0

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua shughuli za kukuza miche ya michikichi, katika kitalu kilichopo kwenye Gereza la Kwitanga katika ziara iliyolenga kukagua maendeleo ya zao chikichi mkoani Kigoma, Mei 23, 2020 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua shughuli za kukuza miche ya michikichi, katika kitalu kilichopo kwenye Gereza la Kwitanga, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya zao chikichi mkoani Kigoma hivi karibuni 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akigawa mce bora wa mchikichi kwa mmoja wa wakulima ikiwa ni uzainduzi rasmi wa zoezi la upandaji michikichi kwenye mkoa wa Kigoma kwa lengo la kufufua zao hilo.

Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

 …………………………………………………………………………………

Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza adhma yake ya kufufua zao la michikichi kwa kugawa bure miche bora milioni 1.8 kwa wakulima mkoani Kigoma.

Akizindua rasmi zoezi la ugawaji na upandaji michikichi jana (23.05.2020) mjini Kigoma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema serikali imelenga kuhamasisha uzalishaji mkubwa wa zao la michikichi ili kuondokana na upungufu wa mafuta ya kula nchini.

“ Miche hii milioni 1.8 ni kwa ajili ya wakulima wa mkoa wa Kigoma,jitokezeni kuandaa mashamba na kisha serikali itawapa bure miche ya michikichi ili ifikiapo mwezi Octoba wakati wa mvua mpande shambani” alisisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alifanya uzinduzi rasmi wa kupanda mche wa mchikichi na kugawa kwa wakulima na vikundi vya AMCOS katika Gereza la Kwitanga na kambi ya 821 Bulombora JKT wilaya ya Kigoma alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja.

Majaliwa aliongeza kusema nchi kwa sasa inalazimika kuagiza mafuta ya mawese toka nje na kutumia zaidi ya shilingi Bilioni 445  wakati Tanzania ina adhi nzuri inayofaa kwa zao hilo.

Uzinduzi huo wa upandaji miche bora ya michikichi umefuatia agizo la Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 kuitaka serikali kufufua zao hilo mkoani Kigoma kwani linastawi vema .

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba alimpongeza Rais wa Awamu ya Tano Dkt.John Pombe Magufuli kwa kuiwezesha wizara kupata fedha shilingi Bilioni 10.8 zilizotumika kuzalisha miche milioni 1.8 ya michikichi kupitia taasisi ya Utafiti TARI na ASA.

Mgumba aliongeza kusema wizara itahakikisha inafikia lengo la kuzalisha miche zaidi ya milioni 15 ili isambazwe kote nchini na wakulima wengi wazalishe zao la michikichi. 

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliagiza Halmashauri za Mkoa wa Kigoma kuwaelimisha wakulima waanze kuondoa miti ya michikichi iliyozeeka kwa awamu na kupanda mipya yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha mawese ili kuongeza tija.

Mwisho.