Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo akiongea na Wakuu wa Vyuo vikuu nchini (hawapo pichani) katika Kikao cha kuweka mkakati wa pamoja wa namna ya kufikia malengo pindi vyuo vitakapofunguliwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo, Marasi na Maprovosti Tanzania (CVCPT), Prof. Raphael Chibunda akitoa ufafanuzi wa mipango waliyoiweka ya kuwezesha kufungua vyuo bila changamoto.
Baadhi ya Wakuu wa Vyuo wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao cha kuweka mkakati wa pamoja kuelekea kufungua Vyuo Juni 1, 2020 kilichofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Vyuo vikuu nchini mara baada ya kumaliza Kikao cha kuweka mkakati wa pamoja wa namna ya kufikia malengo pindi vyuo vitakapofunguliwa kilichofanyika jijini Dodoma
………………………………………………………………………………….
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewakutanisha Wakuu wa Vyuo Vikuu vyote nchini kwa lengo la kuweka mkakati wa pamoja wa namna ya kufikia malengo ya ufundishaji na ukamilishaji wa Mitaala pindi Vyuo vitakapofunguliwa Juni 1, 2020.
Akifungua kikao hicho Katibu Mkuu wa Wizara Ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema pamoja na mambo mengine watakubaliana namna bora ya kuhakikisha vyuo vinafidia muda wa masomo uliopotea na kukamilisha mihula bila kuathiri taaluma.
Mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni kuhakikisha vyuo vinawasilisha nyaraka zote muhimu ili wanafunzi wapate Mikopo yao mapema vyuo vitakapofunguliwa.
“Hakikisheni katika vyuo vyenu mnachagua maafisa mikopo ambao watatoa ushirikiano mzuri kwa wanafunzi ili kusiwe na malalamiko wakati wa kushughulikia mikopo yao,” alisisitiza Dkt. Akwilapo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo, Marasi na Maprovosti Tanzania (CVCPT) ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda amesema wanaishukuru Wizara kwa kuitisha kikao hicho ili kuweka mipango kwa pamoja utakaowasaidia kufungua vyuo bila changamoto na kwamba vyuo tayari vimejipanga kuhakisha Jumuiya za Vyuo zinakuwa salama dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya huku wakiendelea na masomo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Abdul-Razaq Badru amesema Bodi imejipanga kutoa mikopo kwa wanafunzi kwa wakati kwa kushirikiana na vyuo huku akivishauri vyuo hivyo kushirikiana na uongozi wa wanafunzi wakati wa zoezi la utoaji mikopo ili kurahisisha utekelezaji wa kazi hiyo.