…………………………………………………………………………………………
Wadau na wafanyabiashara nchini wamesisitizwa kupata vibali vya vipimo vya mionzi vinavyotolewa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwa njia ya mfumo wa kieletroni kila mara wanapoingiza na kusafirisha bidhaa ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Idara ya Ufundi na Kinga ya Mionzi wa TAEC, Bwana Yesaya Sungita katika mahojiano maalumu kuhusiana na utoaji wa vibali hivyo unaofanyika sasa kwa njia ya mtandao.
Utoaji wa vibali hivyo kwa njia ya mtandao umeanza tokea tarehe moja mwezi Aprili mwaka huu ambapo kwasasa wadau na wafanyabiashara wanapaswa kuwasilisha maombi yao ya vibali kwa kutumia mtandao uitwao rac.taec.go.tz ambapo wateja wote watapaswa kujaza fomu kwa njia ya mtandao na kuwasilisha kwa ajili ya kupata vibali vyao.
Sungita amesema kuwa tangu kuanza kwa utoaji huo wa vibali kwa njia ya mtandao, umesaidia sana kurahisisha kazi na kupunguza mzigo wateja katika kupoteza muda ambapo kwasasa ndani ya saa mbili hadi nne baada ya kulipia na kuwasilisha sampuli mteja anaweza kupata kibali chake tofauti na zamani ambapo ilikuwa ikichukua takribani muda wa siku moja hadi tatu kwa mteja kupata kibali.
“Kubwa hapa wateja wanapaswa kujaza taarifa zenye usahihi ambazo hazitaleta mkanganyiko wakati wataalamu wanaotoa vibali watakavyopitia kabla ya kuidhinisha kwenye mtandao” alisemaSungita.
Ameongeza kuwa awali iliwalazimu wafanyabishara kutumia muda mwingi kufika katika ofisi za TAEC kwa ajili ya kuwasilisha nyaraka zao na sampuli za bidhaa na kwamba sasa urahisi umepatika na nakuongeza tija katika utoaji wa vibali na kwamba umeondoa usumbufu kwa wadau katika upatakanaji wa vibali hivyo.
Sungita amesema kuwa kwa kutumia mfumo huu mteja atapaswa kuomba kibali moja kwa moja kupitia katika mfumo na kupewa gharama stahili na kuwa baada ya malipo kukamilika mteja ataweza kupata kibali chake kupitia mfumo huo.
Ameongeza kuwa kwa sasa wateja hawahitajiki tena kutoka mikoani ili kuleta sampuli za kupimwa katika ofisi za makao makuu ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, kwani maboresho makubwa yamefanyika katika ofisi za kanda na mipakani kwa kuweka vifaa vya kupimia, hivyo mteja atachagua eneo husika analoona ni karibu kwake tofauti na zamani ambapo ilikuwa lazima sampuli zote ziletwe Arusha makao makuu ili kufanyiwa vipimo hivyo.
Pia Bw. Sungita amesema kuwa mfumo huu wa uombaji na utoaji wa vibali vya mionzi kwa njia ya mtandao unatarajiwa kusaidia kuondoa uwezekano wa maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa covid 19, kwa wadau na wateja wa TAEC kutokana na kupunguza msongomano usio wa lazima kwa kufika katika ofisi za TAEC.