Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza leo Jijini Dodoma na Waandishi wa Habari kuhusu mfumo utakaotumika katika michezo ya ligi huku akitangaza vituo viwili vitakavyotumika jiji la Dar es Salaam zitachezewa ligi mbili Ligi Kuu pamoja na kombe la shirikisho la Azam huku jiji la Mwanza Ligi Daraja la kwanza pamoja na Ligi Daraja la pili.
…………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Serikali imetoa utaratibu namna ligi itakavyoendeshwa katika kipindi hiki inarejea kutoka katika mapumziko baada ya kusimamishwa ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Harrison Mwakyembe amesema ligi nne pekee ambazo ni ligi kuu, kombe la shirikisho, ligi daraja la kwanza na la pili ndizo zitaendelea lakini si kwa utaratibu uliozoeleka kwa kila timu kuwa kwenye uwanja wake.
Amesema wameamua kutenga vituo viwili kimoja kikiwa Dar es saalam na Mkoa wa Mwanza, ili kuzuia timu kusafiri kwenda mikoa mbalimbali hii ni kutokana na vilabu vingi kutokuwa na hali nzuri ya kiuchumi.
“Kwa Mkoa wa Dar es saalam hii itakuwa kwa ligi kuu tu, ambapo viwanja vitatu vitatumika, uwanja wa Uhuru, uwanja wa Taifa na uwanja wa Chamazi isipokuwa uwanja wa Taifa utatumika kwa masharti isizidi michezo mitatu kwa wiki”
“Na Mkoa wa Mwanza utatumika kwa ligi daraja la kwanza na ligi daraja la pili na viwanja vitakavyotumika ni Uwanja wa CCM Kirumba na uwanja wa nyamagana Jijini humo” amesema Waziri Mwakyembe.
Aidha amesema katika michezo hiyo hawataruhusu mashabiki kuingia uwanjani ili kuruhusu nafasi na kila timu itaruhusiwa kuingia na viongozi kadhaa na kila wachezaji wanapoingia uwanjani ni lazima wapimwe.
Aidha amesema baraza la michezo pia watakuwepo kuhakiki vipimo ili kusitokee hujuma wakati wa upimaji wa wachezaji wa kila timu hasa kwa wale watakao hisiwa kuwa na joto lililozidi.
“Serikali ipo makini isitokee hujuma ikaonekana kagere kapima akaonekana joto arobaini, morrson arobaini na moja hii sio sawa tutakuwepo kuhakiki” amesema.
Aidha ameitaka BMT kukaa na mashirikisho mengine kuona namna jinsi yatakavyoweza kuendesha ligi au michezo yao bila kuharibu taratibu na kanuni za afya.