Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya akiimba wimbo wa maombolezo kwa hisia kwenye mazishi ya aliyekuwa Katibu mwenezi wa CCM Wilayani Simanjiro marehemu Sumleck Ole Sendeka aliyezikwa kijijini kwao Losokonoi Kata ya Naberera.
******************************
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya amempongeza Rais John Magufuli kwa hatua yake ya kuruhusu maziko kufanyika kwa heshima tofauti na awali watu 10 ndiyo walikuwa wanamzika mtu aliyefariki kipindi hiki cha uwepo wa virusi vya corona.
Ole Millya aliyasema hayo jana kwenye mazishi ya Katibu mwenezi wa CCM Wilayani Simanjiro marehemu Sumleck Ole Sendeka aliyezikwa nyumbani kwao Losokonoi kata ya Naberera.
Alisema hivi sasa ndugu, jamaa na marafiki wanawapa heshima ya kuwafanyia maziko wapendwa wao tofauti na siku chache zilizopita ambapo marehemu alikuwa anazikwa na watu 10.
Alisema anashukuru hilo kwani bila uamuzi wa Rais Magufuli ingelikuwa tatizo na Sumleck angeweza kuzikwa na watu 10 au manispaa ya Arusha kutokana na hofu ya mikusanyiko ya watu kwa kujikinga na corona.
“Mimi kama mbunge kwa niaba ya wananchi wa Simanjiro napenda kumpongeza na kumshukuru Rais Magufuli kwa kutoa ruhusa ya maziko ya heshima kwani bila hivyo wasingeweza kumzika mpendwa wao,” alisema Ole Millya.
Alisema uamuzi huo wa Rais Magufuli umewanufaisha wananchi wa eneo hilo kushuhudia safari ya mwisho ya katibu mwenezi wa CCM Simanjiro.
“Rais Magufuli ameonyesha yeye ni mcha Mungu ndiyo sababu akatoa ruhusa kwa makanisa na misikiti kuendelea na kufanya ibada na watu kutoa heshima za mwisho kwa wapendwa wao waliopoteza maisha,” alisema Ole Millya.
Hata hivyo, alimpongeza mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula kwa kusimama kidete kuhakikisha familia za wafugaji zilizokuwa zimetoka nje ya nchi zinakaa mahali na kupimwa kama wameambukizwa corona.
“Niwapongeze viongozi wa wilaya kwa kulibeba hilo kwani wananchi waliishi bila hofu japokuwa kulikuwa na tatizo la baadhi ya watu kuwa na corona,” alisema Ole Millya.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka alisema anawashukuru viongozi mbalimbali wa CCM na serikali waliompa pole na kushiriki kwenye msiba wa mdogo wake marehemu Sumleck.
Ole Sendeka alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa kusimama kidete kuhakikisha anaongoza mapambano ya corona hadi mataifa mengine yanaiga anavyofanya.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula alisema pamoja na corona kupungua bado wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari ili wasipate maambukizi mapya.
Linna Ole Sendeka alisema marehemu Sumleck alizaliwa mwaka 1968 na kufariki Mei 16 mwaka huu na alikuwa anasumbuliwa na tatizo la kifua.