Home Mchanganyiko WAKANDARASI WA MIRADI YA MAJI WAPEWA ONYO KALI

WAKANDARASI WA MIRADI YA MAJI WAPEWA ONYO KALI

0

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Manyoni, Mhandisi Gabriel Ngongi
akisoma taarifa ya Mradi wa Maji wa Kintinku-Lisulile kwa Naibu
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso katika Halmashauri ya Wilaya ya
Manyoni, mkoani Singida.

Mitambo ya kusukuma maji ya Mradi wa Maji wa Maji wa Kintinku- Lisulile katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida.

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akitoa onyo kwa mwakilishi wa mkandarasi Kampuni ya M/S Nangai Engineering Ltd baada ya kukagua na kutoridhishwa na maendeleo ya kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Vijiji 6 vya Songambele, Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi katika Halmashauri ya Itigi, mkoani Singida.

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akitoa maalezo baada ya kukagua ujenzi wa Mradi wa Maji wa Vijiji 6 vya Songambele, Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi katika Halmashauri ya Itigi, mkoani Singida. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa.

Ujenzi wa moja ya matenki mawili ya maji yenye ujazo wa lita 200,000 kwa ajili ya Mradi wa Maji wa Vijiji 6 vya Songambele, Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi katika Halmashauri ya Itigi, mkoani Singida.

Ujenzi wa tenki la maji na nyumba ya pampu kwa ajili ya Mradi wa Maji wa Maji wa Kintinku-Lisulile katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida.

********************************

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewaagiza wakandarasi wote walioitelekeza miradi ya maji kwa sababu ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona kurudi kwenye maeneo yao ya kazi kuendelea na utekelezaji haraka.

Naibu Waziri Aweso amekasirishwa na utendaji wa wakandarasi wa Kampuni za M/S Nangai Engineering Ltd na M/S Nipo Africa Engineering Ltd wanaosuasua katika utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa Maji wa Vijiji 6 vya Songambele, Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi katika Halmashauri ya Itigi, mkoani Singida.

 

Akisema kuwa zaidi ya Sh. Bilioni 1.3 zimeshatolewa kwenye mradi huo na maendeleo ya kazi yakiwa nyuma ya ratiba na kukwamisha lengo la mradi unaotarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 31,000 katika vijiji 6
vinavyozunguka mji wa Itigi.

 

“Kipindi hiki cha Ugonjwa wa Corona, ni haki kwa kila mtanzania kupata huduma toshelevu ya maji ili kulinda afya za wananchi dhidi ya ugonjwa huu, pia Serikali inachukua hatua madhubuti kukamilisha haraka miradi ya
maji ili iweze kutoa huduma ambayo ni haki ya kila mtanzania’’, amesema Naibu Waziri Aweso.

 

“Nawaagiza wakandarasi wote walioitelekeza miradi ya maji kwa sababu ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona warudi kwenye maeneo yao ya kazi na kukamilisha ujenzi wa miradi haraka, ni kweli ugonjwa upo tunachotakiwa
ni kuchukua tahadhari lakini kazi zisisimame, atakayekaidi agizo la Serikali tutamchukulia hatua za kisheria kwa kuwa atakuwa anatukwamisha”, ameonya Naibu Waziri Aweso.

 

Akiwatahadharisha wakandarasi kuacha tabia ya kuitelekeza miradi kwa muda mrefu, na kuonekana kwenye maeneo ya kazi pindi viongozi wa wizara wanapokuwa wakifanya ziara za kukagua miradi hiyo kwa lengo la kutaka kuridhisha viongozi hao.

 

“Niwatake watumishi wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) kuwabana wakandarasi wafanye kazi zao usiku na mchana na kutoa taarifa za mara kwa mara zinazohusu changamoto zote
za kiutekelezaji ziweze kutatuliwa haraka ili miradi isikwame”, Naibu Waziri Aweso amesema.

 

Mapema Naibu Waziri Aweso alitembelea Mradi wa Maji wa Kintinku-Lisulile katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kuelekeza mkandarasi alipwe Sh. Milioni 370 anazodai aweze kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi
wa mradi huo, ambapo asilimia 10 imebaki ili uweze kukamilika.

 

Akisema wakati wa usomaji wa Bajeti ya Wizara ya Maji, wabunge walizungumzia sana juu ya kukamilika kwa miradi ya maji katika Wilaya za Manyoni na Itigi, na kutoa ahadi ya kutembelea miradi hiyo kabla ya Bajeti
Kuu kusomwa ili kuchukua hatua za haraka za kuikamilisha.

 

Akisoma taarifa ya Mradi wa Maji wa Vijiji 6 katika Halmashauri ya Itigi, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Manyoni, Mhandisi Gabriel Ngongi amesema ujenzi wa mradi unasimamiwa na RUWASA, utekelezaji wake ulianza Mwezi Disemba, 2018 na unategemea kukamilika ifikapo Mwezi Juni, 2020 kwa gharama za zaidi ya Sh. Bilioni 2.6.

 

Amesema miongoni wa kazi za ujenzi ni ujenzi wa matenki mawili ya maji yenye ujazo wa lita 200,000, tenki la maji la lita 100,000, vituo vya kuchotea maji 40 na vioski 16 vya kutolea huduma, lambo la kuhudumia wanyama pamoja na kazi nyingine.