********************************
Chama cha mapinduzi mkoa wa Njombe kimempokea na kumkabidhi kadi ya uanachama aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa NCCR Mageuzi,Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti Chadema,Mjumbe wa kamati ya UKAWA na Kampeni meneja wa nafasi ya makamu wa rais UKAWA Juju Maltin Danda.
Akiweka bayana sababu ya kujiunga na chama cha mapinduzi baada ya kufanya siasa katika vyama vya upinzani kwa nyakati tofauti Juju Danda amesema ni kutokana na utendaji mzuri wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ambaye amefanikiwa kuzika agenda za ufisadi na ubadhirifu ambazo zilikuwa zinabebwa na upinzani.
Aidha Amesema ameshindwa kuzuia hisia zake kwa kitendo cha rais kufanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo reli,barabara,umeme na mingine bila kuyumbishwa na propaganda za mataifa ya nje na vyama vya upinzani.
Kuhusu vyama vya upinzani Danda amesema vyama hivyo vimeishiwa kabisa agenda na badala yake vimebaki kufanya biashara na kutawaliwa na uozo mkubwa katika shughuli zake za kisiasa.
Amesema kilichobaki katika vyama hivyo ni kutengeneza wana harakati badala ya kufanya siasa zenye lengo la kujenga taifa letu hali ambayo imesababisha kushindwa kuvulia na kuamua kujiunga na chama tawala ambacho kimeendelea kuwa mfano barani Africa na dunia kwa ujumla.
“Mimi ni mwanasiasa ambaye nimejitahidi kutembea kwa nguvu zangu milima na mabonde kuieneza chadema na kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa vya vyuo vikuu nyanda za juu kusini kueneza chadema vyuoni na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa lakini kinachoendelea sasa kwenye vya upinzani ni uozo wa hali ya juu sasa na kufanya kushindwa kuvumilia” Amesem Juju Danda.
Awali katibu wa siasa na uenezi CCM mkoa wa Njombe Erasto Ngole amesema chama cha mapinduzi kimempata mwanasiasa muhimu na mashughuri katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi na kueleza namna alivyokuwa mwiba kwa chama tawala kwa zaidi ya chaguzi tano zilizofanyika kipindi cha nyuma.
Ngome amesema katika kipindi cha kampeni Juju Danda amekuwa licha ya viongozi wake kufanya kampeni kwa kutumia helkopta na maghari ya kifahari lakini yeye amekuwa akifanya kwa kutumia baiskeli na wakati mwingine kwa mguu jambo na kufanikiwa kukonga mioyo ya watu.
“NCCR Mageuzi imekuwa na vijiji na mitaa inavyotawala katika mkoa wa Njombe kutokana na ushawishi na kazi kubwa iliyofanywa na bwana Danda hivyo CCM imepata mtu muhimu katika kipindi hiki”Amesema Erasto Ngole
Akizungumza mara baada ya kumkabidhi kadi ya uanachama bwana Danda mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Njombe Jasel Mwamwala amesema kitendo cha kurejea nyumbani kimeonyesha ukomavu mkubwa na kwamba hakuna budi kumpokea kwa mikono miwili mwana huyo mpotevu .
Mwamwala amesema kadiri siku zinavyosogea chama cha mapinduzi kimezidi kuwa na mvuto kutokana na kutambua thamani na utu wa watu na kudai kwamba wiki moja iliyopita chama hicho kiliwapokea madiwani wane wilayani Makete ambao walikihama chama cha demokrasia na maendeleo chadema kwa madai ya kutofurahishwa na mwenendo wa chama hicho.
“Kutokana na nguvu na ushawishi mkubwa wa Ndugu Danda alipaswa kupokelewa na katibu mkuu jijini Dar es salaam lakini kutokana na uzalendo wa mtu huyu akaamua kupokelewa Njombe” Amesema Jasel Mwamwala mwenyekiti wa CCM mkoa.