Ofisa Miradi kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Furaha Kessy akiwasikiliza Wauguzi wa Kituo cha Afya Uhuru, Tumaini Majoji na Zawadi Rashid namna wanavyotoa huduma za chanjo kwa kuzingatia mwongozo wa kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, wao na wateja wanaowahudumia.
……………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Maalum – Morogoro
Watoa huduma za chanjo katika vituo vya afya nchini wamehimizwa kuzingatia mwongozo wa kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona na kuendelea kutoa chanjo kwa watoto na wasichana kwa wenye umri wa miaka 14 inavyostahili kwa mujibu wa ratiba zao.
Rai hiyo imetolewa leo mjini hapa na Ofisa Miradi kutoka Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, Furaha Kessy alipozungumza na watoa huduma hao katika Kituo cha Afya Sabasaba, Kituo cha Afya Mafiga na Kituo cha Afya Uhuru wakati wa ziara ya kukagua namna wanavyotoa huduma huku wakijikinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo.
“Ndiyo tupo kwenye janga la Corona lakini ni muhimu mno chanjo kuendelea kutolewa kwa watoto kama ambavyo inatakiwa kulingana na ratiba zao.
“Pia kuna kundi la wasichana wenye umri wa miaka 14 ambao wanastahili kupata chanjo ya HPV inayokinga dhidi ya maambukizi ya kirusi hicho kinachosababisha saratani ya kizazi.
“Kundi hili awali wapo ambao walikuwa wakipatiwa chanjo shuleni, lakini kwa sababu ya Corona shule zimefungwa, lazima tujue namna gani hawa tutawapata kuwapa chanjo ya pili ili kukamilisha ratiba zao,” ametoa rai.
Kessy ameongeza “Wataalamu wanapaswa kutoa chanjo hizo huku wazingatia mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo, Jinsia, Wazee na Watoto wa kujikinga ili wasipate maambukizi wao huku wakiwakinga pia wateja wanaowahudumia.
“Zingatieni kujikinga vema, chanjo ziendelee kutolewa na tunazo, kundi la wasichana wale lazima nalo tulifikie ili tusije tukajikuta siku zijazo tunapata milipuko ya magonjwa mengine ambayo yanaweza kuzuilika kwa chanjo, hili muhimu tulizingatie,” amesisitiza.
Muuguzi wa Kituo cha Afya Uhuru, Tumaini Majoji amesema awali janga hilo lilipotangaza kuwapo nchini walikuwa na hofu jinsi watakavyoweza kuhudumia wateja huku nao wakibaki kuwa salama bila kupata maambukizi kwa sababu ni ugonjwa mpya na hawakuwa na uelewa wa kutosha jinsi ya kujikinga.
“Uongozi wa kituo umetupatia elimu jinsi ya kujikinga na timu maalum ya kutoa elimu ya kujikinga pia ilikuja kutuelimisha, sasa tunaelewa, hatuna hofu tena, tunazingatia mbinu za kujikinga na tunatoa huduma za chanjo na elimu kwa jamii jinsi ya kujikinga pia,” amesema.
Muuguzi wa Kituo cha Afya Sabasaba, Celina Daffa amesema wanaendelea kutoa huduma na kwamba kwa wiki hupokea wateja wapatao 50 na kuwapa chanjo mbalimbali.
Mratibu wa Huduma za Chanjo wa Manispaa hiyo, Hidaya Omari amesema wana jumla ya vituo 47 vinavyotoa huduma za chanjo kila siku.
“Katika vituo vinavyotoa huduma ya uzazi (kujifungua) na kwa vituo ambavyo havitoi huduma ya kujifungua vyenyewe hutoa kwa siku tano pekee katika wiki,” amebainisha.
Ameongeza “Huduma zinaendelea isipokuwa tulipata changamoto kwa kundi hili la wasichana wa miaka 14 kwa sababu chanjo zilikuwa zinatolewa shule lakini zilipofungwa kutokana na Corona kuna ambao bado hatujaweza kuwapata kuwapa chanjo.
“Kutokana na hali hiyo, jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika, sasa tumekubaliana kuanza kuwatumia watoa huduma za afya ngazi ya jamii (CHW’s) kuwahimiza wasichana hawa kwenda katika vituo vya afya kupatiwa chanjo maana tunazo,” amesisitiza.
Amesema makadirio yao kwa mwaka ni kuwafikia wasichana wapatao 4,762 wa umri wa miaka 14 kuwapatia chanjo hiyo ikiwa ni sawa na wasichana 395 kwa mwezi.
“Katika chanjo ya kwanza tulifanikiwa kwa kiwango cha asilimia 100 kulifikia kundi hili, katika kipindi cha mwaka huu Januari hadi Machi, tumepata changamoto tumeweza kuwafikia asilimia 80 tu, kwa sababu ya janga la Corona, shule zimefungwa na sasa wapo nyumbani,” amebainisha.