Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akiongea na viongozi wa Chama cha Wasiona Tanzania (hawapo pichani) kabla ya kuwakabidhi msaada wa vifaa vya
kujikinga na Corona.Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akiongea na Mratibu wa Idara ya Maendeleo ya Vijana na Chipukizi ya Chama cha Wasiona Tanzania, Bw. Omari Itambu (Kulia) na Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Zumba (kushoto). Viongozi hao walialikwa katika ofisi za OSHA, Kinondoni, Dar es Salaam kwa ajili ya kukabidhiwa msaada wa vifaa vya kujikinga na Corona.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akiwakabidhi viongozi wa Chama cha Wasioona Tanzania baadhi ya vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Corona
vilivyotolewa na taasisi yake katika kulisadia kundi hilo.
***********************************
Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umetoa msaada wa vifaa kinga kwa wanachama wa Chama cha Wasioona Tanzania ili kuwawezesha kujikinga na
ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) unaosababishwa na virusi vya corona.
Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa kwa viongozi wa chama hicho ni pamoja na vitakasa mikono (sanitizers), barakoa, ndoo za kunawia mikono kwa maji tiririka pamoja na sabuni za maji.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa viongozi wa chama, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema OSHA kama taasisi ya umma yenye jukumu la kuhakikisha
maeneo ya kazi yanakuwa salama, wameguswa na changamoto kubwa inayolikabili kundi hilo maalum katika kujikinga na ungonjwa wa Corona.
“Sote tunafahamu kwamba dunia na nchi yetu ipo katika mapambano dhidi ya janga la Corona ambapo kila mtu anahimizwa kuchukua tahadhari dhidi ya virusi hatari vya
Corona kwa kutekeleza maelekezo mbali mbali yanayotolewa na wataalam wetu wa afya, hivyo kwakutambua changamoto zinazowakumba wenzetu wasioona tumeona ni vema tukawasaidia baadhi ya vifaa kinga muhimu,” alieleza Mtendaji Mkuu.
Kiongozi huyo mkuu wa OSHA aliongeza kuwa watu wasioona wanakuwa na wakati mgumu zaidi katika kujikinga na Corona kutokana na hali yao ambapo mara nyingi hulazimika kugusana na watu wengine hata wasiowafahamu husasan wanapohitaji msaada wa kuvushwa barabara au kuongozwa toka eneo moja kwenda jingine.
“Miongoni mwa vifaa tulivyotoa ni vitakasa mikono ambavyo vipo katika chupa ndogo ndogo ambazo walengwa wataweza kutembea nazo na hivyo kuwawezesha kutakasa mikono yao kila wanapolazimika kugusana na watu wanaowaongoza au wanapokuwa
wameshika vitu mbali mbali,” alifafanua Bi. Mwenda.
Aidha, aliwaomba wadau wengine kujitokeza na kutoa misaada zaidi kwa makundi ya watu wenye ulemavu ili nao waweze kujikinga na kuendelea kushiriki katika shughuli
mbali mbali za ujenzi wa Taifa.
Akitoa neno la shukrani mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo muhimu, Mratibu wa Idara ya Maendeleo ya Vijana na Chipukizi ya Chama cha Wasiona Tanzania, Bw.
Omari Itambu, amewashukuru OSHA kwa masaada huo muhimu kwa wanachama wake.
“Kwanza, tunamshukuru Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwakututoa hofu kwamba tunaweza kupambana na ugonjwa huku tukiendelea kuchapa kazi ili kujipatia riziki.
Aidha, niwashukuru OSHA chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) kwa msaada wa vifaa hivi muhimu kwetu katika mapambano dhidi ya janga la Corona kwani imekuwa taasisi ya kwanza kutusaidia kati ya taasisi nyingi ambazo tuzilipelekea maombi ya vifaa hivi. Tunawaomba wadau wengine waendelee kutusaidia
vifaa hivi kwani mahitaji bado ni mengi,” alisema Bw. Itambu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Zumba alisema: “Kwa niaba ya wasioona wa mkoa wa Dar es Salaam, tunapenda
kuwashukuru OSHA kwa msaada huu wa vifaa vya kujikinga na ugonjwa hatari wa Corona na tungependa pia kutoa wito kwa watu wengine waweze kutusaidia pia kwani watu tusioona tupo katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa ugonjwa huu.”