…………………………………………………………………………………
MKURUGENZI wa Taasisi ya Munanta Med Company Ltd na wataalamu wa afya wametembea jamii za pembezoni ikiwemo wafugaji wa Tarafa ya Engaranaibo Wilayani Longido Mkoani Arusha kwa kuwapatia vifaa na elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ili kuhakikisha nao wanaepuka kupata tatizo hilo.
Munanta Med pamoja na kutoa elimu hiyo kwenye masoko na minada pia, maofisa watendaji na wenyeviti wa vijiji, viongozi wa kimila, waganga wa jadi na wakunga wamepatiwa mafunzo ya kupambana na corona.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk Juma Muna akizungumza jana wakati akitoa mafunzo hayo alisema lengo ni kuongeza uelewa hasa kwa jamii zilizopo pembezoni ambapo elimu haijawafikia zaidi.
Dk Muna alisema eneo la tarafa ya Engaranaibo lipo vijijini mpakani mwa nchi ya Kenya na wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro na Namanga mkoani Arusha hivyo elimu hiyo inatakiwa kutolewa kwa ukubwa zaidi.
Alisema jamii hizo za wafugaji hukutana kwenye mnada uliopo Engaranaibo, bila kuwapa elimu ya kujikinga na corona wengi wao wataathirika ndiyo sababu wakafika kuwaelimisha.
Alisema ikiwa ni miezi kadhaa tangu corona iingie nchini ni wajibu wa wadau kutoa elimu ya afya katika kujikinga na janga hilo ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na kuvaa barakoa na kutokaribiana.
“Ukishawapa elimu hii viongozi wa kimila, wakunga wa jadi na waganga, tegemea jamii ya wafugaji kwa ujumla itanufaika kwani huwa wanawasikiliza mno viongozi wao tofauti tungewaeleza sisi wenyewe,” alisema Dk Muna.
Alisema pamoja na elimu hiyo pia walitoa baadhi ya vifaa vya kujikinga na corona ikiwemo sabuni za kunawia mikono lita 65, ndoo 13 za kuweka maji tiririka na barakoa 100.
“Pia tumewaeleza kuwa maji yanapaswa kuosha mikono walau kwa sekunde 20 kukaa umbali wa mita moja na kufuata miongozo yote inayotolewa na serikali wa idara ya afya,” alisema Dk Muna.
Mkazi wa eneo hilo, Yamati Ole Motika alishukuru taasisi ya Munanta Med kwa kuwapa elimu ya namna ya kuepuka maambukizi na pia vifaa vya kujikinga na corona.
Motika alisema jamii za pembezoni huwa zinasahauliwa kwenye masuala mbalimbali kutokana na jiografia yao ila wanashukuru kwa wao kukumbukwa.
Alitoa ombi kwa wadau mbalimbali wajitokeze kuwasaidia kwani jamii ya wafugaji waliopo pembezoni nao wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma hasa kipindi hiki cha kupambana na corona.