***********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Matango ni matunda yanayojulikana kwa kuwa na faida ya kuondoa sumu mwilini na wengine wamekuwa wakiyatumia kwa namna nyingi.
Asili ya kilimo cha matango inaaminika kuwa ni kaskazini magharibi mwa India ambako yamekuwa yakilimwa kwa zaidi ya miaka thelathini sasa. Hata hivyo kwa sasa, matango, hustawishwa katika sehemu nyingi za kitropiki. Matunda yake hukatwa katwa na kuliwa kama achali, au kachumbari, au huwekwa kwenye siki na pia hupikwa na kuliwa.
Katika nchi yetu ya Tanzania matango hulimwa katika mikoa ifuatayo: Tanga, Morogoro, Mbeya, Lindi, Mtwara na Pwani ambako kuna jua la kutosha. Pia mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kilimo cha matango hukubali.
Aina Za Matango
Zipo aina nyingi za matango lakini hutofautiana kwa umbo na rangi. Aina zinazojulika na kulimwa zaidi hapa kwetu ni: Colorad, Telegraph, Palmetto, Chicago, Pickling, Straight 8 na Marketer.
Matumizi
Matango hutumiwa kama matunda na pia ni aina ya mboga ambayo huongeza vitamin A, C na maji mwilini. Matunda haya yanaweza kutumika pia kama saladi wakati wa mlo.
Upandaji
Ni vizuri kama mkulima wa matango akapanda mbegu moja kwa moja shambani, sia mbegu moja kiasi cha sentimita moja chini ya udongo, na umbali kati ya mbegu na mbegu usipungue sentimita 30 na zaidi.
Sehemu ya kupandia iwe na jua la kutosha kwani matango huhitaji kiasi cha jua kisichopungua masaa 6 – 8 kwa siku, mwagilia maji ya kutosha angalau mara moja kwa siku hasa nyakati za jioni. Hii itasaidia ukuaji bora wa mazao yako hivyo kukuhakikishia mavuno mazuri.
Mbolea
Kabla ya kupanda weka viganja 2 vya mbolea ya zizi katika kila shimo na changanya na udongo. Pia weka kg 100 za NPK kwa hekta moja. Wiki tatu hadi nne baada ya kupanda: Weka mbolea ya CAN kwa kiwango cha kijiko kimoja cha mezani kwa kila mmea (= gramu 10 kwa mmea). Mbolea ni muhmu sana katika kilimo cha matango kwani zao hili pia hutumia chakula kingi kutoka ardhini, hivyo muhimu kuweka samadi au mboji mara kwa mara ili kuongeza chakula cha mmea.
Palizi
Palilia kila wakati magugu yanapojitokeza, ni muhimu sana, hii husaidia kuepuka magonjwa na kushindania chakula kati ya zao na magugu. Palizi hutakiwa kufanywa kwa kutumia jembe la mkono ili kuepuka kuharibu mizizi.
KUVUNA
Matango huwa tayari kuvunwa kuanzia siku 50 hadi 60, yaani mwezi mmoja na nusu hadi miwili baada ya kupanda, na pia matunda yanatakiwa kuwa na urefu wa sentimita 15 mpaka 20, urefu pia unaweza kutofautiana kulingana na aina ya matango yaliyopandwa. Baada ya mvuno wa kwanza mkulima anaweza subiri wiki tatu kabla ya kuvuna mvuno wa pili.
SOKO
Matango yana soko kubwa ndani na nje ya nchi yetu. Biashara ya matango ndani ya nchi yanauzwa rejareja kwa bei ya shilingi mia mbili hadi mia tano kwa tango moja. Hata hivo bei hutofautiana kulingana na upatikanaji au uzalishaji wa matango wa mahali husika. Pia unaweza kuuza kwenye migahawa, mahoteli na cafeteria.
Wajasiliamali wengi wameweza kunufaika na kilimo hichi cha matango na kuweza kupata soko kwa haraka na gharama nzuri kabisa katika mauzo yake.