Mhandisi Yusuph kutoka kampuni ya Yapi Merkezi (wa kwanza kushoto) akiilezea timu ya Maafisa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi, ramani ya ujenzi wa kituo kikuu cha Morogoro pamoja shughuli zitakazokuwa zinafanyika katika kituo hicho ili wataalam hao waweze kuandaa mpango wa kuendeleza eneo hilo kulingana na shughuli zitakazokuwa zinatekelezwa katika kituo hicho. Kituo hiki cha Morogoro kimezungukwa na shamba la mkongwe pamoja na makazi ya watu.
Timu ya Maafisa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi, wakijadiliana na wahandisi wa ujenzi reli ya kissasa (SGR) jinsi gani wanaweza kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania kuendeleza maeneo yanayozunguka vituo kwa kuzingatia shughuli na mahitaji ya vituo hivyo vya treni ili kuepuka ujenzi holela katika maeneo yote yatakayokuwa na vituo vikubwa na vya kati vya treni ya mwendo kasi.
Mhandisi Hamza Said (mwenye kofia) kutoka Shirika la Reli Tanzania akiwaelezea wataalam wa Mipango Miji Kutoka Wizara ya Ardhi ramani ya ujenzi wa kituo kikuu cha Dar es Salaam na shughuli zitakazokuwa zinafanyika katika kituo hicho. Kituo cha Dar es Salaam ndiyo kituo kikubwa zaidi na kituo namba moja cha treni ya mwendo kasi. Treni ya mwendo kasi na ile ya kawaida zote zitakuwa zinaanzia safari zake katika kituo hiki cha Dar es Salaam ambapo treni ya mwendo kasi itakuwa inapita juu na ile ya kawaida itakuwa inapita chini bila kuathiri shughuli za maendeleo za kila siku.
………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaandaa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika maeneo yote yanayozunguka vituo vya treni ya mwendo kasi (SGR) ili kuwezesha ardhi ya maeneo hayo kuendelezwa kwa kuzingatia shughuli zitakazokuwa zikifanyika sambamba na mahitaji muhimu kwa watumiaji wa vituo hivyo.
Hayo yalibainishwa juzi na Afisa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Edward Mpanda wakati timu ya Wataalamu kutoka Idara ya Mipango Miji ilipotembelea mradi huo katika eneo la Kilimanjaro mkoani Morogoro, sehemu kinapojengwa kituo kikuu cha treni ya mwendo kasi.
Alisema, Wizara yake imejipanga kwa kushirikiana na Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi pamoja na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha inaandaa mpango maalum wa kuendeleza Ardhi inayozunguka vituo vya treni ya SGR ambayo ujenzi wake ulishaanza.
Kwa mujibu wa Mpanda, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Tume ya Matumizi bora ya Ardhi itahakikisha pia reli ya kisasa (SGR) inatunzwa kwa kuzingatia mpango uliowekwa ili kuleta ufanisi na maendeleo kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo.
‘‘Kama Wizara isiposimamia uendelezaji Ardhi inayozunguka eneo la mradi, basi kila mmoja atakuja na ujenzi wake bila kujali athari itakayotokea kutokana na shughuli zitakazokuwa zikiendelea katika vituo hivyo vya treni’’ alisema Mpanda.
Aidha, Afisa huyo wa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema Usimamiaji wa uendelezaji Ardhi katika maeneo yanayozunguka mradi wa ujenzi reli ya kisasa (SGR) utasaidia kuondoa ujenzi holela katika maeneo hayo na kuweka miundo mbinu itakayokuwa na tija kwa watumiaji hasa katika vituo vyote vikubwa na vya kati
Kwa upande wake Mhandisi Hamza Said kutoka Shirika la Reli Tanzania, aliishukuru timu ya Wataalamu wa Mipango Miji kwa kutembelea mradi huo na kubainisha kuwa Wizara ya Ardhi bado haijachelewa kuandaa mipango yake na kusisitiza muda bado upo kwa kuwa ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea.
‘‘Kuweka mpango wa kuendeleza maeneo kwenye vituo vya treni ya mwendo kasi itakuwa na faida kwa sababu maeneo hayo yatakuwa na tija kwa watumishi watakaokuwa wakihudumia vituo hivyo lakini pia na kwa wasafiri wa treni ya mwendo ya kasi na ile ya kawaida’’ alisema Mhandisi Hamza
Timu ya Wataalamu wa Mipango Miji kutoka Wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilitembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa lengo la kubaini aina ya Ardhi inayozunguka maeneo inakojengwa ili kuweka mikakati ya jinsi ya kuyaendeleza maeneo hayo.
Mfumo wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayojengwa na Kampuni ya Yapi Merkezi ya nchini Uturuki umegawanywa katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza yenye vituo sita inatoka Dar es Salaam hadi Morogoro huku awamu ya pili ikianzia Morogoro hadi Makutopora Manyoni mkoani Singida ikijumuisha vituo tisa.
————————————–MWISHO—————————————————–