Home Mchanganyiko ZAIDI YA MILIONI ISHIRINI KUTUMIKA UJENZI WA NYUMBA YA MKAZI WA WETE...

ZAIDI YA MILIONI ISHIRINI KUTUMIKA UJENZI WA NYUMBA YA MKAZI WA WETE ANAISHI NA WATOTO YATIMA

0

………………………………………………………………………….

Na Masanja Mabula ,PEMBA .

ZAIDI ya shilingi Milioni Ishirini zinatarajia kutumika kujenga nyumba ya Mwanamvua Omar Hassan  mkaazi wa Shehia ya Maziwani Wete mwenye watoto sita yatima baada ya nyumba yake kuanguka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Nyumba hiyo ya kisasa itajengwa na Jumuiya ya Awadood Charitable Group yenye makao yake visiwani Zanzibar inayosaidia mayatima baada ya kuguswa na hali hiyo na kuahidi kumjengea nyumba  ya kisasa mama huyo ambaye ni mjane.

Akikabidhi msaada wa magodoro,Mashuka pamoja na vyakula kwa familia 20 ambazo nyumba zao zimeanguka kutokana na mvua huko Maziwani , Mwakilishi wa Jumuiya hiyo Yakoub Khalfan alisema ujenzi wa nyumba hiyo utaanza hivi karibuni.

“Tumeguswa na tukio hili na sisi kama Jumuiya tutamjngea nyumb ya kisasa yenye thamani ya shilingi milioni ishirini na moja (21,000,000) ujenzi ambao utaanza ndani ya mwezi huu”alifahamisha.

Kwa upande wake Mwanamvua Omar Hassan alipongeza msaada huo.

Alisema baada ya nyumba yake kuanguka ,yeye na familia yake  ya watoto sita mayatima, wamepata hifadhi katika majengo ya skuli ya Maziwani.

“Naishukuru sana Jumuiya hii kwa kunijali na kuamua kunijengea nyumba itasaidia kuishi mimi na watoto wangu ambao ni mayatima”alisema.

Naye sheha wa shehia hiyo Bi mwanaidi Khamis Alela  alisema uwamuzi ulichukuliwa na Jumuiya hiyo kwani utapunguza adha na shida anazopata yeye na watoto wake.

Mkuu wa wilaya ya Wete Kepteni Khatib Khamis Mwandini akizungumza baada ya kupokea msaada huo kutoka  Jumuiya ya Awadood alitumia fursa hiyo kuwataka wahisani kuendelea kuwasaidia wananchi waliopata maafa ya mvua.

“Serikali inatambua na kuthamini juhudi zinazochukuliwa na asasi za kiraia na kwamba itaendelea kushirikiana nazo katika kusaidia kukabiliana na changamoto za jamii”alisisitiza.

Alifahamisha kuwa kiasi ya familia mia mbili wilayani humo zimeathirika na mvua huku familia 10 zikiwa zimehifadhiwa katika majengo ya skuli na kituo cha afya Maziwani na nyengine kuhifadhiwa na majirani.