Kanisa Kuu la Kristu Mfalme Anglikana katika Manispaa ya Mpanda
Askofu Mathayo Kasagara aliyevaa msalaba akiwa na baadhi ya waumini (picha kwa hisani ya Maktaba)
………………………………………………………………………….
Na Zilpa Joseph, Katavi
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ziwa Rukwa Mathayo Kasagara amewasisitiza waumini wa kanisa kuu la Kristo Mfalme lililopo katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi kuona umuhimu wa kuvaa barakoa wakiwa katika shughuli mbalimbali hasa kanisani wakiwa ibadani ama katika mazoezi ya kwaya
Ametoa rai hiyo katika ibada ya pili inayoendeshwa na kanisa hilo ambapo amewaeleza waumini hao kuwa ugonjwa wa korona bado upo na kusisitiza kuendelea kuchukua tahadhari
“Haijalishi kama hivi sasa hatupati matangazo ya mara kwa mara ya mwenendo wa ugonjwa huo hapa nchini, kwamba wagonjwa wapya wangapi, wangapi wamekufa na wangapi wamepona” alisema Askofu Kasagara
Askofu Kasagara amesema kwa sasa wamevunja ibada za watoto zinazojulikana kama Sunday School kwa lengo la kuwakinga watoto na kuwataka wazazi kufika na watoto wao kanisani na sio kuwaacha waje wenyewe
“Watoto wanapendana, wakikutana wanacheza na kushikana, hivyo niwashauri wazazi wasiwaache watoto peke yao” alisema
Pia amewataka wachungaji na wahudumu wote wa kanisa kuvaa barakoa wakati wote wa ibada na hata wanapokuwa wakitoa huduma mbalimbali kwa waumini
“Mimi hapa nimevaa barakoa, nahubiri na barakoa yangu, ni kwa sababu hiki kipasa sauti (microphone) tunatumia kimoja kwa zaidi ya mtu mmoja! Kwahiyo hata waimbaji niwatake mvae barakoa hata wakati wa kuimba” alisema askofu Kasagara