Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Elizabeth Kitundu akitoa maagizo mbalimbali ya Serikali kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
************************************
Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Elizabeth Kitundu amewataka maofisa biashara, watendaji wa kata na vijiji wa eneo hilo kuwakamata wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei ya juu tofauti na bei elekezi ya sh2,700 kwa kilo.
Kitundu aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Babati katika makao makuu mapya kata ya Dareda.
Alisema maofisa biashara na maofisa watendaji wa kata na vijiji wanapaswa kufuatilia wafanyabiashara hao na kuwachukulia hatua za kisheria ambao bado wanaopandisha bei ya sukari.
Alisema serikali imeshatangaza bei elekezi ya sh2,700 hivyo wafanyabiashara watakaoendelea kuuza bei ya juu tofauti na hiyo wanatakiwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Baadhi ya wananchi wa hapa Babati wamefikisha malalamiko yao ofisini kwangu kuwa bado kuna wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei ya juu ya sh2,700 hivyo mkachukue hatua juu ya hilo,” alisema Kitundu.
Alisema mfanyabiashara atakayekwenda kinyume na maagizo ya serikali akichukuliwa hatua za kisheria asilaumu kwani alikiuka utaratibu ndiyo sababu akafuatiliwa.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto, Tumaini Magessa alifanya ziara ya kushtukiza na kamati ya ulinzi na usalama kwenye maduka ya mji mdogo wa Kibaya ili kubaini bei ya sukari.
Magessa aliwapa onyo wafanyabiashara wa sukari wa eneo hilo wanaouza bei ya juu tofauti na maelekezo ya serikali ya sh2,700 kwa kilo mkoani Manyara.
“Wanaoendelea kuuza sukari kwa sh3,500 kwa kilo mnajitafutia matatizo kwani serikali itawachukulia hatua, uzeni kwa bei inayotakiwa ya sh2,700 na siyo vinginevyo,” alisema.
Mkazi wa mtaa wa Nyunguu mjini Babati Rukia Salao alisema bado kuna changamoto ya baadhi ya maduka kuuza sukari kwa sh3,500 hali inayowaumiza walaji.
Salao alisema mfanyabiashara hata mmoja angekamatwa na kulala mahabusu wengine wangetii amri halali ya serikali ya kuuza kilo moja kwa sh2,700.