*****************************
Na Emmanuel Shilatu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amuapisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mbunge wa Iramba Magharibi) kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Hafla iliyofanyika Wilayani Chato Mkoani Geita , Mei 03, 2020. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba anachukua nafasi ya Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga aliyefariki dunia tarehe 01 Mei, 2020.
Kwenye hotuba yake Rais Magufuli ameongea mengi yenye tija ila baadhi ya Watu wanaleta siasa.
Baadhi ya Watu wanasema Rais Magufuli amedanganya juu ya upimaji wa Papai kwa sababu Papai halina damu! Watu hawa wanashindwa kuelewa sampuli za upimaji wa virusi vya Corona ni za maji maji mfano mate, makamasi na si damu. Watu hawa “vilaza” wanaodai Rais amepotosha wanataka kutuaminisha Papai halina majimaji yatakayoweza kutumika kama sampuli ya upimaji?
Wengine wanasema Rais Magufuli hajui tatizo wala ukubwa wa Corona nchini. Watu hawa wanashindwa kuelewa Urais ni taasisi ambapo yeye anapokea taarifa yeyote ile anayoitaka muda wowote ule.
Rais huyu wanayemsema hajui tatizo la Corona nchini ndio Rais huyu huyu alisitisha zoezi la uwashaji Mwenge, maadhimisho ya sherehe za Muungano na maadhimisho ya sherehe za Wafanyakazi na kuelekeza fedha hizo ziende kupambana na ugonjwa wa Covid 19. Huu ni ushahidi tosha kuwa analitambua tatizo lilivyo na ukubwa wake.
Ni katika Serikali yake ametoa maelekezo ya Kiserikali ya kufunga shule za msingi na vyuo; kusitisha michezo yote nchini; kutoa maelekezo wageni wote wanaoingia nchini wawekwe karantini kwa siku 14. Hizi zote ni baadhi ya jitihada za Serikali kutambua tatizo na harakati katika kupambana na tatizo la virusi vya Corona nchini.
Wengineo baadhi wanasema Rais Magufuli amekimbia tatizo kwa kwenda kujichimbia kijijini kwao Chato. Watu hawa wanasahau ya kuwa Rais hana mipaka ya ukaaji, mipaka ya kufanya kazi kijiografia na ndio maana hata tatizo la ugonjwa wa Corona aliliweka wazi akiwa barabarani kwenye ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa Ubungo interchange na wala hakuwa ofisini ama Ikulu na utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa barabarani ya kukabiliana na tatizo yakaanza mara moja. Hiyo ndio nguvu na mamlaka ya Rais neno lake analotamka hata kama akiwa uchochoroni ni agizo la kufanyiwa kazi mara moja.
Ni Rais Magufuli huyu huyu ambaye hatujawahi kusikia akisafiri safiri nje ya nchi amebaki ndani akikabiliana vyema na matatizo ya ujambazi, mauaji ya Kibiti, Panyaroad na hadi sasa imebaki historia na tatizo kuisha. Rais Magufuli ameyaweza magumu yote hayo yakiwemo ya ufisadi nchini hata hili la Corona nalo pia amelimudu na tatizo litaweza kuisha endapo tutashirikiana kwa pamoja.
Ndugu zangu, ni jukumu letu sote kuhakikisha tunashikamana kwa pamoja kuhakikisha tunapambana vilivyo na adui Covid 19 kwa kuhakikisha tunaepuka mikusanyiko, hatushikani mikono, tunavaa barakoa, tunanawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji yanayotiririka na si kuweka pembeni maelekezo ya Wataalamu wa afya na kuchukulia suala hili kisiasa, hatumkomoi Rais Magufuli bali tunajikomoa sisi wenyewe na jamii yetu.
Hatuwezi kupambana na ugonjwa huu kwa kuchafuana, kutishana na kutiana hofu. Ni wakati wa kusimama imara tusijiyumbishe kwani hili litapita kama yalivyopita mengine.
Tuache kupeana hofu, tumeishinda hii vita tayari kwani Serikali ya Rais Magufuli imepambana vilivyo na tatizo hili na si kubwa kulinganisha na nchi nyinginezo lilivyo.
Narudia tena kusema tumeishinda hii vita tayari, tuungane kwa pamoja kukabiliana na tatizo. Tusimame na Rais Magufuli, tusimame na ukweli. Vita tumeishinda, tutavuka salama daraja.