WAZIRI wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Isimani Mkoani Iringa Mh. William Lukuvi amekabidhi kwa wananchi wa jimbo hilo jumla ya ndoo 270 maalum za kunawia mikono kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha Ugonjwa wa Covid 19.
Akizungumza wakati wa kukabidhi ndoo hizo Katibu wa mbunge huyo Thom Malenga alisema kuwa vifaa hivyo vimetolewa kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa jimbo la Isimani kutekeleza kwa vitendo ushauri wa wizara ya afya nchini inayomtaka kila mwananchi kunawa mara kwa mara ili kujiepusha na maambukizi ya Corona
Katibu huyo aliwahimiza wananchi kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya na kuzitumia ndoo hizo kwa kutakasa mikono kila wakati kwa kuwa ndio moja ya kinga ambayo inaweza kuepuka kukumbwa na maambukizi ya virusi hivyo ambavyo vimekuwa hatari kwa maisha ya Binadam
Malenga alisema kuwa mbunge ametoa ndoo maalumu nne kwa kila kijiji ambacho kipo katika jimbo la Isimani kwa lengo la kusaidia katika maeneo yenye mikusanyiko na maeneo maalum kama ofisi za kijiji,virabu vya pombe na sehemu za kuabudia.
“Leo tumekabidhi ndoo maalum zenye uwezo wa kubeba lita Ishirini kwa mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela kwa lengo la kusaidia kujikinga na virusi vya Corona,kinga bora kuliko tiba hii ndio sababu ya mbunge kutoa msaada huu” alisema Malenga
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela alisema mbunge wa jimbo la Isimani William Lukuvi amekuwa mstari wa Mbele kuhakikisha anawasaidia wananchi wake kwa kila jambo linapotokea huku akiwahimiza wabunge na viongozi wengine kuiga mfano wa kujitolewa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.
“Jukumu letu ni kuhakikisha tunawatafutia sabuni wananchi ambao hawawezi kununua ili kuwasaidia kujikinga na virusi vya Corona” alisema Kasesela
Kasesela alisema kuwa ndoo hizo maalum zinaghama kubwa hivyo wananchi wanapaswa kuzitunza na kuendelea kumheshimu mbunge huyo kwa juhudi ambazo amekuwa akizitoa kuhakikisha wananchi wanapata mahitaji muhimu kwa maendeleo.
Hadi kufikia hii leo wilaya ya Iringa haijapata mgonjwa yeyote yule mwenye maambukizi ya virusi vya Corona hivyo bado wananchi wapo salama na wanapaswa kuendelea kujikinga na virusi hivyo.
Naye mwenyekiti wa umoja wa vijana Wilaya ya Iringa vijijini Makala Mapessah alimpongeza mbunge huyo kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha wananchi wa jimbo la Isimani wanakuwa salama kwa kujikinga na virusi vya Corona.