MJUMBE wa mkutano mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Iringa Vijijini Arifu Abri akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kukabidhi msaada uliopokelewa na mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.( Picha na Denis Mlowe).
*******************************
NA DENIS MLOWE, IRINGA
MJUMBE wa mkutano mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Iringa Vijijini Arifu Abri ametoa msaada wa chakula tani tatu kwa ajili ya wahanga wa mafuriko wa kijiji cha Isele kilichoko tarafa ya Pawaga wilaya ya Iringa vijijini mkoanbi Iringa kwa kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya chakula.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, Arifu Abri alisema kuwa changamoto wanayokabiliana nayo wananchi wa kijiji hicho imepelekea kujitoa kuwasaidia watu wenye mahitaji muhimu ili kuokoa maisha yao madhara waliyopata kutokana na mafuriko hayo.
Alisema alipata taarifa ya wananchi wa kitongoji cha Mbingama kijiji cha Isele kuwa wamepatwa na mafuriko kutokana na kunyesha kwa mvua nyingi msimu huu wa kilimo na kusabaisha hasara kubwa kwa wananchi waliokuwa wanaishi katika eneo hilo lililotokea mafuriko na kutegemea zaidi kilimo kwa ajili ya maisha.
Alisema kuwa moja ya mahitaji ambayo wahanga wa mafuriko wa kitongoji cha Mbingama ni wananchi asilimia kubwa kukosa chakula cha kila siku hivyo ndio maana msaada wangu nimejielekeza kwenye kutoa chakula zaidi ambapo utawasaidia kwa kipindi hiki cha mafuriko.
“Najua kuna wadau wengine wameshatoa baadhi ya msaada kulingana na mahitaji hata hivyo kwa upande wangu mimi nimeamua kutoa chakula kulingana na mahitaji ambayo nimeona wanahitaji wahanga wa mafuriko wa kitongoji cha Mbingama kijiji cha Isele Tarafa ya Pawaga” alisema
Abri alitoa wito kwa wadau wengine kuendelea kujitokeza kuwasaidia wahanga hao wa mafuriko katika kitongoji cha Mbingama ili kuwasaidia kurudi kwenye maisha ambayo walikuwa wameyazoe hapo awali kulingana na shughuli ambazo walikuwa wanazifanya kupa riziki zao.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela mara baada ya kupokea msaada huo alimshukuru mjumbe wa mkutano mkuu ccm taifaArifu kwa msaada huo kwa kuwa umekuja katika wakati mwafaka kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo wananchi hao.
Aidha Kasesela alitoa wito kwa wadau kujitokeza zaidi kuwasaidia wananchi hao ambao licha ya changamoto ya chakula wanakabiliwa na changamoto ya nguo, makazi, madawa kwa lengo la kuweza kuondokana na hali hiyo.