………………………………………………………………………………….
Na Emmanuel J. Shilatu
Ni miaka 56 imetimia tangu jahazi lililowabeba Watanganyika na Wazanzibar liweke historia ya kung’oa nanga mara baada ya Jamhuri Muungano wa Tanzania kuzaliwa rasmi mnamo April 26,1964. Hii ilitokana na ujasiri, ushupavu na nia ya dhati waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar).
Hatua hiyo ilifikiwa kutokana na mtiririko wa kimazingira na mahusiano ambayo yalishabihiana kama sio kufanana kabisa kwa pande zote mbili (Tanganyika na Zanzibar). Zipo sababu za kijiografia, kisayansi, kitamaduni na kihistoria zilizochangia huu muungano wetu.
Kutokana na sababu za kijiografia na kisayansi inaaminika kabisa kwamba Visiwa vya Zanzibar (Pemba na Unguja) vilikuwa vimeungana na hata kushikamana kwa pamoja pembezoni mwa pwani ya ardhi ya Tanganyika. Hivyo tangu awali tulikuwa ni kitu kimoja, tulio katika ardhi moja na ya pamoja.
Pia kuna historia (isiyo na shaka) ya muingiliano wa kiutamaduni baina ya Wakazi wa Tanganyika na Zanzibar ambapo hali nzima ya kuoa ama kuolewa ilizidi kushamiri baina yao.
Halikadhalika harakati za kudai ukombozi wa uhuru wetu ili tuweze kujitawala wenyewe kutoka kwa dudu la wakoloni nazo zilichangia kutuunganisha. Inaaminika (na ndiyo ilivyo) ya kuwa asilimia kubwa ya Wazanzibar walishiriki kwenye harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Mwingereza ambapo kutokana na nia, ushupavu na nguvu ya pamoja walifanikiwa kupata Uhuru wa Tanganyika mnamo Desemba 9, 1961.
Lakini pia licha ya asilimia kubwa ya Wazanzibar kushiriki katika mchakato wa Mapinduzi ya Zanzibar lakini pia kulikuwepo na asilimia kubwa ya mchango wa ushiriki kutoka kwa Watanganyika. Hatimaye matunda yake yalionekana ya mapinduzi matukufu yaliyofikia kilele katika uwanja wa Gombani Pemba yaliyofanyika Jamhuri 12, 1964, baada ya kuchoshwa na hila na ghiliba za Waarabu uliotamalaki visiwani humo kwa zaidi ya karne mbili na hatimaye waliwaacha wazalendo watwana katika ardhi yao.
Pia tusisahau lengo na nia ya dhati aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere ya kutaka kuiunganisha Afrika mzima kwa hatua lakini jitihada zake zilianza kuzaa matunda ambayo hayatakaa yatokee tena Afrika kwa kuiunganisha Tanganyika na Zanzibar.
Mnamo April 22, 1964, Maraisi wa nchi hizi mbili ambazo sasa zinaunda Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (wa Jamhuri ya Tanganyika) na Abeid Amani Karume (wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar ) walitia sahihi Mkataba wa kimataifa wa kuunganisha nchi zao, unaojulikana kama “Hati ya Muungano” (Articles of union) na hivyo kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ama United Republic of Tanganyika and Zanzibar (URTZ) ambao ni muungano sahihi kabisa kisheria na unaotambulika Kikatiba.
Siku ya Jumatatu ya tarehe 26 Aprili, 1964 viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee kwa nia ama lengo moja tu la kubadilishana “Hati za Muungano”.
Wananchi wa Tanzania walipiga kura kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa kwanza kabisa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwaka 1965.
Kama nilivyodokeza kwamba Muungano wa Tanzania ulifikiwa kwa kutiwa sahihi mkataba unaoitwa Hati ya Muungano (Articles of the Union) na wakuu wa nchi hizi mbili, Mwalimu Nyerere (Tanganyika) na Abeid Karume (Zanzibar) Aprili 22,1964 na kuridhiwa na mabunge ya nchi hizo Aprili 25, 1964 na hatimaye kuwa sheria ya Muungano ya (Acts of Union) ya mwaka 1964.
Kimsingi sheria ya Muungano ndiyo iliyoanzisha na ndiyo iliyopewa haki ya chombo cha kikatiba kinachodhibiti katiba zote mbili za Serikali ya Muungano.
Mwanzoni kabisa Hati ya Muungano (Articles of Union) iliyomo ndani ya sheria ya Muungano iliorodhesha na hata kudadavua mambo 11 ya Muungano. Mambo hayo ni kama vile:- Mambo ya nchi za nje, Ulinzi na usalama (lakini si usalama wa Taifa); Polisi, Uraia, uhamiaji, mikopo na biashara za nchi za nje, utumishi katika serikali ya Muungano, kodi ya mapato, usimamizi wa fedha, Bandari, Usafiri wa anga, Posta na simu.
Kwa nia safi na malengo mazuri yanayojitokeza Hati ya Muungano imekuwa ikiboreshwa zaidi kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele kwa malengo kusudi ya kuleta umoja, mshikamano, amani na utulivu wetu ule ule tulioanza nao awali na halikadhalika maridhiko yanayoendelea kuufanya Muungano huu uendelee kudumu hadi hii kesho.
Ndio maana mtu timamu hatoshangaa sana kuona Hati ya Muungano ikiendelea kuboreshwa kila siku (na itaendelea hivyo) ambapo ilianzia na mambo 11 ambapo hii leo yamefikia takribani 23.
Mengineyo ama baadhi ya yale yalioongezeka ni kama vile;- Noti; Elimu ya juu,; Maliasili na mafuta (mafuta) yasiyochujwa, bidhaa za mafuta na gesi asilia , ya mwaka 1968; Baraza la Mitihani ya Taifa; utafiti; utabiri wa hali ya hewa; Takwimu,; Mahakama ya Rufaa ya juu ya mwaka 1979; pamoja na uandikishwaji wa vyama vya kisiasa .
Tusisahau mwaka 1965 iliundwa katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (The Interim Constitution of The United Republic of Tanzania) mpaka kufikia mwaka 1977 ndipo ilipoundwa katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo inaendesha nchi hadi sasa.
Muungano huu tulionao unawafanya wale wageni, mataifa ya nje na watu wote wenye hila, donge, roho ya korosho kuogopa kutugusa na kutuvuruga kutokana na kuwepo kwa nguvu kubwa ya umoja, ushirikiano na mshikamano baina yetu.
Muungano huu wetu unatupatia fursa kubwa ya uhuru wa kusafiri kwa pande zote iwe ni bara ama ni visiwani. Leo hii ni rahisi sana kwa mtu wa bara kwenda Visiwani na hata wale wa Visiwani kuja Bara kwa uhuru zaidi kwani Uhuru huo wa uwepo wa nafasi hiyo umeshalipiwa na huu Muungano wetu tulionao.
Kutokana na uwepo wa uhuru wa kusafiri usio na mipaka baina yetu, pia Muungano wetu tulionao unazidi kutuongezea fursa na nafasi zaidi ya uwanja mpana wa ufanyaji biashara. Hali hii imesababisha uwepo wa mzunguko mkubwa wa pesa ndani yetu kwani si jambo la ajabu kuona pesa zikitoka Visiwani (Zanzibar) kuja Bara (Tanganyika) kupitia mabadilishano ya bidhaa kama vile nafaka, kahawa, matunda, vipuri vya magari na kadhalika.
Pia si jambo geni tena kwa sasa kuona pesa zikivuka Bahari na kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya ufanyaji ama ununuzi wa biashara kama vile Magari, nazi, Karafuu, Tende na kadhalika.
Muungano huu unatuzidishia fursa ya mianya ya uwanja mpana tena usio na kikomo wa ufanyaji biashara, Muungano huu hautubagui ama kutojulisha au kuwa na upendeleo wa upatikanaji wa Elimu bora, huduma za kijamii bora, Muungano hautugawi wala kuwa na upendeleo bali umejaa uwiano sahihi wa upatikanaji wa mabo yote ya msingi yaliyomo ndani ya “Hati ya Muungano” (Articles of union). Muungano huu ni nguzo imara katika muktadha mzima wa nyanja za kimaisha yetu.
Ni ukweli uliodhahiri kuwa haitakaa itokee Muungano kama huu (wa Tanganyika na Zanzibar) hapa Barani Afrika umoja ushirikiano, ushikamano, amani na utulivu ni sehemu mojawapo ya manufaa ya Muungano huu.
Hakika, historia tunailinda na kuiheshimu. Njia mojawapo ya kuwaenzi vyema waasisi wetu ni kwa kuudumisha Muungano wetu ambao ni urithi wa aina yake waliotuachia. Watanzania yatupasa tuenzi Muungano wetu kwa kuulinda na kuudumisha kwa vitendo kwani ni nguzo na fahari ya kipekee na ya aina yake Barani Afrika.