Mdau wa maendeleo mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo (mwenye njano)akiwa katika picha ya pamoja na watu wasioona baada ya kuwakabidhi msaada wa Barakao 200 na sanitezer 40 kwa ajili ya chama wasioona manispaa ya Iringa kwa lengo la kupambana na kuenea kwa virusi vya Corona. (Picha na Denis Mlowe)
……………………………………………………………………………………..
NA DENIS MLOWE,IRINGA
JAMII imeshauriwa kuwashika mkono watu wenye ulemavu wa macho hasa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya Corona COVID 19 kwani wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali kutokana na hali zao.
Hayo yamezungumzwa na mganga mkuu wa Manispaa ya Iringa, Dk. Jesca Leba wakati wa mafunzo na kupokea msaada wa Barakao 200 na Sanitezer 40 kwa ajili ya walemavu wa macho uliotolewa na mdau wa maendeleo mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo kuweza kuwasaidia kwa ajili ya mapambano dhidi ya Corona.
Dk. Leba alisema kwamba kutokana na hali walizonazo walemavu wa macho kuna umuhimu mkubwa wa jamii kuwa nao sambamba kwani wako katika hali ya hatari zaidi kutokana na hali zao za kutokuona hivyo elimu na kuwaongoza namna ya kunawa mikono itasaidia katika mapambano hayo.
Alisema kuwa kama manispaa wametoa mafunzo kwa walemavu na wataendelea kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali ya walemavu kwa ajili ya kushikwa mkono kwani changamoto kubwa kwenye vyombo vya kunawia mikono wanashindwa kuelewa mahali ilipo.
“Kwa kweli kuna changamoto kubwa kwa walemavu na ndio maana tumeamua kufanya mafunzo kwao tena maalum kwa kundi la walemavu wa macho na tutafanya mafunzo haya kwa makundi yote kwa sababu watu wanaohitaji kushikwa mikono katika kuwaongoza” alisema
Aidha katika mafunzo hayo, Dk Leba aliwataka walemavu wa macho kuepuka kushika macho, pua na mdomo kwa mikono isiyo safi kwa sababu mikono ni rahisi kubeba vimelea vya maradhi na kuzingatia ustaarabu wa kuzuia pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya.
Alisema kuwa endapo binaamu atahisi kuwa na mafua makali, homa, kikohozi na kushindwa kuhema nenda hospitali kupata msaada wa kitaalamu na kuepuka kuwa sehemu yenye msongamano kama vyombo vya usafiri, maduka na maeneo yenye mgandamizo wa hewa.
Kwa upande wake , Mdau wa maendeleo ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa UVccm mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo alisema kuwa msaada una lengo la kuwasaidia walemavu wa macho kwani wamesaulika sana katika mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya Corona.
Alisema kuwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu jamii inatakiwa kuungana kwani hali ya kuleta au kutaka sifa kisiasa sio wakati wake na kumpongeza Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuri kwa kuwa mstari wa mbele katika kupambana dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona.
Aliwataka wakosoaji dhidi ya mapambano haya watumie lugha za staha na kuacha tabia ya kushutumiana ila ni wakati wa kuungana kuweza kumtokomeza adui aliyeko mbele ya jamii kwa sasa ambaye ni virusi vya corona.
Naye mwenyekiti wa chama wa Wasioona manispaa ya Iringa, Huruma Maketa alisema kuwa wamejifunza vizuri zaidi tofauti na mwanzo kuhusu gonjwa la Corona na kumshukuru mdau wa maendeleo Fadhili Ngajilo kwa kutoa msaada barakao na sanitizer kwa walemavu wa macho.
Aidha alishukuru mafunzo waliyopatiwa ya kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya Corona kwani mafunzo hayo yalikuwa muhimu kwa jamii ya wasioona hivyo elimu hiyo watatumia vyema kuepukana na kuambukizwa na virusi vya corona.