Mkurugenzi wa FM Abri, Alifu Abri (kulia)akimkabidhi ndoo maalum za kunawia mikono na sabuni (sanitezer) diwani wa kata ya Kising’a iliyoko jimbo la Ismani ikiwa ni kuungana na serikali katika mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona – Covid 19. (picha na Denis Mlowe)
Mkurugenzi wa FM Abri, Alifu Abri akiwa na diwani wa kata ya Kising’a na watendaji wa kata hiyo mara baada ya kukabidhi msaada wa vifaa vya kunawia mikono kwenye kata hiyo.
Baadhi ya ndoo maalum zilitolewa na Mkurugenzi wa kampuni ya Fm Abri (Famari) kwa kata ya Kising’a iliyoko jimbo la Ismani wilaya ya Iringa vijijini .
********************************
NA DENIS MLOWE, IRINGA
WAZAZI na Walezi nchini wametakiwa kuwa makini na Watoto katika kipindi hiki ambapo shule zimefungwa kutokana na agizo la serikali na wakati ambao nchi iko katika mapambano dhidi ya Virusi vya COVID 19 vinavyosababisha ugonjwa wa Corona.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya. F.M Abri, Alifu Abri wakati wa kugawa msaada wa ndoo maalum za kunawia mikono sabuni za kutakasa mikono, fedha za ununuzi wa barakoa kwa kata ya Kising’a iliyoko Iringa vijijini vilivyopokelewa na diwani wa kata hiyo Litta Mlagala kuwa kuwalea Watoto katika mazingira bora kuepukana na kupata virusi hivyo.
Alisema kuwa Vifaa hivyo ambavyo vimetolewa na kampuni hiyo vitasambazwa katika vituo vyote vya afya, kwenye misikiti na kanisani vina thamani ya sh. Milioni 1.2 vitaendana na elimu kwa jamii ili kuweza kuwa na tabia ya kunawa mikono mara kwa mara na kuomba dua kwa MUNGU kuweza kuepukana na maambukizi Zaidi.
Alisema kuwa Watoto wengi wakati huu wamekuwa wakitumia muda wa shule kufunga kucheza michezo mbalimbali hali ambayo inahatarisha kwa kiasi kikubwa usalama wa Maisha yao na kuweza kupata au kuambukizwa virusi vya korona.
Alisema hivi sasa hapa Iringa na Tanzania kwa ujumla kuna watu kadhaa ambao ni wameambukizwa virus vya corona hivyo ni muhimu kwa wazazi kuwa makini na Watoto hasa katika mikusanyiko wanayokutana na kuwataka kuwapa elimu ya kubaki ndani kuliko michezo ambayo inasababisha mikusanyiko ambayo serikali imepiga marufuku.
Alisema zipo changamoto mbali mbali katika ulezi wa Watoto hao,lakini ni vyema wazazi wakaongeza juhudi katika malezi ili kupata watoto walio bora hapo baadae na kuondokana na kuambukizwa.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kising’a iliyoko jimbo la Ismani, Lita Mlagala akizungumza kwa masikitiko, alisema wakati mwengine watoto wanakufa kutokana na mambo madogo madogo tu ikiwemo kuwaacha bila uangalizi maalum.
Alisema kuwa katika kata hiyo Watoto wawili wamepoteza Maisha kwa matukio tofauti ikiwemo mmoja kuzama kwenye bwawa na mwingine kupata ajali ya bodaboda hivyo umakini wa wazazi unahitajika sana katika kuwalea na kuwakataza kuzurura.
Alisema kuwa mbaya Zaidi katika kipindi hiki cha janga la Corona ambapo shule zimefungwa Watoto baadhi wamekuwa wakiacha kusoma nyumbani wametumia muda huo kukimbia majumbani na kwenda mijini kufanya kazi mbalimbali.
Mlagala alimshukuru mkurugenzi wa FM Abri , Alifu Abri kwa kwa kuona iko haja ya kutoa msaada huo ambao utasaidia kunusuru Maisha ya wakazi wa Kising’a kwa kutoa msaada na kutaka elimu Zaidi itolewe kwa jamii kuhusu janga la Corona.
“Naamini msaada huu utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupambana dhidi ya virusi vya Corona katika kata yet una umekuja wakati mwafaka kabisa hivyo nakushukuru sana Alifu na naomba msaada wa Barakoa kwa vituo vya afya vya kata hii” alisema
Aidha alitoa wito kwa makampuni na taasisi nyingine kuiga mfano wa mkurugenzi Alifu Abri kwa kutoa misaada mbali mbali ili kusaidia jamii katika kutatua changamoto zinazowakabili hasa katika kipindi hiki ambapo dunia anapambana na virusi vya corona.