Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (Wa pili kutoka kushoto) akiwa kwenye maombi mafupi ya kuliombea taifa dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona muda mfupi kabla ya kuanza kukagua josho la mifugo lililopo mnada wa awali wa Buzirayombo uliopo Wilaya ya Chato Mkoa wa Geita leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akizungumza na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato na wakala wa majengo (TBA) leo kwenye eneo la mnada wa wa awali wa Buzirayombo unapotarajiwa kufanyika ujenzi wa majengo ya kisasa ya mnada wa upili .
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Leonard Mwaisabula akielezea manufaa ya mnada wa upili wa Buzirayombo kwa upande wa halmashauri hiyo pindi utakapoanza kazi wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel leo alipofika Wilayani humo kwa ajili ya kukagua eneo itakapojengwa miundombinu ya mnada huo.
Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA) Mkoa wa Geita Mhandisi Gladys Jeffa mapema leo akifafanua hatua ambazo mpaka sasa ofisi yake imefikia kabla ya kuanza ujenzi wa miundombinu ya mnada wa Upili wa Buzirayombo unaotarajiwa kuanza kabla ya mwezi Julai mwaka huu.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati), Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA) mkoa wa Geita Mhandisi Gladys Jeffa (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Leonard Mwaisabula wakielekea kwenye josho la mifugo lililopo ndani ya mnada wa awali wa Buzirayombo wakati wa ziara yake ya kukagua eneo hilo la mnada leo
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akipokea maelezo ya namna utakavyokuwa mnada wa Upili wa Buzirayombo baada ya kukamilika kwake kutoka kwa Mhandisi wa Wakala wa Majengo (TBA) Bw. David Luoga leo alipofika kwenye eneo hilo kwa ajili ya kukagua.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akisoma maelezo ya kibao cha ufunguzi wa kliniki ya Mifugo iliyopo Wilayani Chato ambako alifika leo kwa ajili ya kukagua miundombinu ya kliniki hiyo inayotarajiwa kukarabatiwa upya kwa ushirikiano baina ya Halmashauri ya Wilaya hiyo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
…………………………………………………………………………….
Na.Mwaandishi wetu,Chato
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka wataalam wa sekta ya mifugo kote nchini watumie muda mwingi kwenda kuwahudumia wafugaji badala ya kukaa ofisini.
Prof. Ole Gabriel ameyasema hayo mara baada ya kufika kukagua moja ya kliniki za mifugo iliyopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita leo ambapo amemshauri Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bw. Leonard Mwaisabula kutenga kiasi cha fedha cha kuanza ukarabati wa kliniki hiyo na Wizara yake itamuunga mkono kwa kukamilisha hatua zilizobaki.
“Ni kweli Wizara ina mpango wa kukarabati kliniki zote za Mifugo hapa nchini lakini kipaumbele chetu cha kwanza ni kwa zile halmashauri ambazo zitakuwa zimeshaanza ukarabati kwa kutumia fedha za mapato yao ya ndani hivyo kama Chato mkianza mapema Wizara pia itawapa kipaumbele na hatimaye muwe mfano kwa wengine” Aliongeza Prof. Ole Gabriel.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Leonard Mwaisabula amesema kuwa halmashauri yake itayafanyia kazi ushauri huo kwa sababu wana shauku kubwa ya kuona kliniki hiyo inafanya kazi.
“Nimepokea ushauri wako Mhe. Katibu Mkuu na kesho tutakutana kwa ajili ya kuangalia mchanganuo wa fedha tulizokuwa tumetenga kwenye idara ya mifugo ili kuona namna tunavyoweza kuanza na ukarabati wa kliniki hii kwa sababu kwetu ina umuhimu Mkubwa sana” Alisema Bw. Mwaisabula.
Mara baada ya kutoka kwenye eneo hilo Prof. Olr Gabriel alielekea kwenye eneo la mnada wa Buzirayombo unapotarajiwa kujengwa mnada mkubwa wa upili ambako alioneshwa kuridhishwa na usanifu wa michoro inayoonesha namna mnada huo utakavyokuwa baada ya kukamilika kwake.
“Lakini pia nimeona eneo hili la mnada litakuwa linajumuisha pande mbili zinazotenganishwa na barabara hivyo Mkurugenzi kwa kushirikiana na Wakala wa Majengo (TBA) ni lazima muangalie namna ya kufanya ili kuhakikisha wananchi wanakuwa salama wakati wote wakiwa kwenye eneo la mnada” Aliongeza Prof. Ole Gabriel.
Pia alipendekeza kutokana na michoro ya mnada huo kuonesha ni wa kisasa ni lazima kuwe na mfumo mzuri wa matangazo ndani ya eneo la mnada, kituo kizuri cha Polisi kitakachofanya kazi kwa saa 24, Mfumo wa kibenki na huduma za afya zitakazowanufaisha wananchi wote watakaokuwa karibu na eneo hilo la mnada, Runinga kubwa itakayoonesha kila kinachoendelea Mnadani hapo na mfumo mzuri wa kuhifadhi idadi na aina ya bidhaa na huduma zinazopatikana mnadani hapo ili kuwe na utaratibu wa kupata taarifa zote muhimu ndani ya muda mfupi
Kwa upande wake Meneja wa TBA Mkoa wa Geita Mhandisi Gladys Jeffa aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano Mkubwa iliowaonesha mpaka sasa ambapo aliahidi kufanya kazi nzuri itakayokamilika kwa wakati.
“Tunataka kuhakikisha mpaka kufika mwisho wa Mwezi Mei tuwe tumekamilisha na kuwasilisha hii hatua ya michoro yote ya mnada huu na tunataka kabla ya kuvuka mwaka huu wa fedha mkandarasi awe site” Alisisitiza Mhandisi Jeffa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Leonard Mwaisabula alisema mradi huo kwao una manufaa makubwa kwa sababu utaongeza kiasi cha makusanyo ya fedha za ndani na hivyo kuiwezesha Halmashauri kuboresha miundombinu ya huduma mbalimbali za jamii kama vile Elimu na afya.