**************************
Baada ya serikali wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe kupokea taarifa kwa raia wema kuwa kuna watu watatu wanaohisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya CORONA wanatarajiwa kuingia wilayani humo wakitokea jijini Dar es salaamu kupitia basi la kampuni la Luwinzo lielekea Ubaruku na kulazimika kuchukua hatua za haraka za kulishikilia basi hilo lilipowasiri mjini Makambako, Hatimae serikali imetoa kauli kufua sintofahamu hiyo.
Akifafanua kuhusu taarifa hizo mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe Comrade Ally Kassinge anasema wananchi walipiga simu katika ofisi yake na kudai kwamba kuna watu watatu wanatoka jijini Dar es salaam kuja wilayani Wanging’ombe katika kijiji cha Ilembula ambao wanahisiwa kuwa na maambukizi ya virus vya CORONA ,taarifa ambazo zilichukuliwa hatua za haraka kwa udharura wake ambapo walilazimika kuhusisha watalaamu wa afya na vyombo vya ulinzi na usalama na kulishikilia basi hilo mpaka vipimo vilipofanyika na kupata taarifa za awali kutoka mtaa waliokuwa wakiishi Jijini Dar es salaam.
Kuhusu matokeo ya uchunguzi wa awali kuhusu watu hao Kassinge pamoja na mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Makambako Alexander Mchone wanasema katika vipimo vya awali hakuna mtu ambaye amebainika kuwa na dalili za ugonjwa huo na kuamua kuliachia gari hilo la abiria kuendelea na shughuli zake za kila siku huku pia rai ikitolewa kwa wananchi kutoa taarifa sahihi pindi wanapohisi kuwepo kwa mtu mwenye maambukizi ya CORONA.
Nae msimamizi wa Kampuni hiyo ya Usafirishaji wa abiria Harid Nyemo anasema ni kweli basi lao lilishikiliwa hadi majira ya saa tisa usiku kutokana na kusambaa kwa taarifa za kubeba watu wanaohiswa kuwa na virus vya CORONA na kudai kwamba baada ya vipimo vya awali kufanyika na kubaini washukiwa hawaja athiriwa ,serikali ikalazimika kuliacha huru basi hilo.