Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akisoma maelezo baada ya kuzindua Muongozo wa Mpango wa Watoa huduma ya Afya ya Jamii, Dar es Salaam jana. Wizara ya Afya imezindua muongozo huwa ikiwa ni muendelezo wa kuendelea kutoa kipaumbele katika kuimarisha huduma za kinga, ikiwemo elimu ya afya na uhamasishaji, lishe, udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na afya ya mama na mtoto.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, Ummy akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Muongozo wa Mpango wa Watoa huduma ya Afya ya Jamii, Dar es Salaam jana. Wizara ya Afya imezindua muongozo huwa ikiwa ni muendelezo wa kuendelea kutoa kipaumbele katika kuimarisha huduma za kinga, ikiwemo elimu ya afya na uhamasishaji, lishe, udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na afya ya mama na mtoto.
……………………………………………………………………………
Serikali ya awamu ya Tano imesema kuwa itaendelea kutoa kipaumbele katika kuimarisha huduma za kinga, ikiwemo elimu ya afya na uhamasishaji, lishe, udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na afya ya mama na mtoto.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu katika uzinduzi wa muongozo wa mpango wa huduma za afya katika jamii na matumizi ya dashibodi ya viashiria vya elimu ya afya kwa umma jijini Dar es Salaam leo.
“Hii itasaidia juhudi za kupunguza mzigo wa gharama za matibabu unaowatesa wananchi na kuongeza matumizi ya serikali katika tiba ya magonjwa yanayoweza kuzuilika au kuepukwa,” alisema waziri.
Alisisitiza kuwa umuhimu wa huduma za kinga ambao umezingatiwa katika Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 na Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya wa Mwaka 2015 – 2020 utakuwa kipaumbele katika maandalizi ya Sera Mpya ya Afya ya Mwaka 2020.
Mkakati huu wa kutumia watoa huduma za afya kwa jamii utawezesha kuwepo kwa huduma imara za kinga katika ngazi zote ikiwemo utoaji elimu ya afya na uhamasishaji kama njia muhimu ya kusaidia jamii zetu kujikinga na magonjwa.
Serikali inatambua kuwa jamii yenye elimu sahihi juu ya vyanzo vya afya bora na masuala yanayoweza kuathiri afya hufanya maamuzi sahihi juu ya mambo yanayohusu afya zao.
Hii itawezesha Taifa letu kuwa na wananchi wenye afya njema wanaochangia katika maendeleo yao, familia zao, jamii wanayoishi na nchi yetu kwa ujumla.
Amesema kuwa serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya ili kufikia malengo ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote yaani Universal Health Coverage ambavyo itajumuisha utoaji elimu ya afya juu ya mambo yahusuyo lishe, afya ya uzazi, watoto na vijana ikijumuisha magonjwa ya mlipuko kama COVID-19 pamoja na magonjwa yasiyoambukiza.
Pia jitihada hizi zinalenga kuhamasisha matumizi ya bima za afya ili kuwawezesha wananchi kutumia huduma mbalimbali za afya wanapohitaji.
Kwa mfano katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita tumeshuhudia ongezeko la idadi ya watu waliopatiwa huduma za magonjwa yasiyoambukizakutoka watu milioni 3.4 (3,386,067) mwaka 2016 hadi wagonjwa Milioni 4.2 (4,190,467) mwaka 2018 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 24 ya wagonjwa hao.
Sambamba na takwimu za wagonjwa, pia tumeshuhudia ongezeko la vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza hadi kufikia asilimia 33 ya vifo vyote nchini kwa mwaka 2017, ambapo jumla ya vifo 134,600 viliripotiwa na kuhusishwa na magonjwa yasiyoambukiza.
Huku vifo vitokanavyo na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu vikichangia kwa asilimia 13, idadi ambayo ni kubwa kuliko ile itokanayo na magonjwa kama Ukimwi, Kifua Kikuu au Malaria.
Waziri Mwalimu alisema kuwa matatizo yote haya yanaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa sana endapo tutaimarisha mifumo ya kutoa elimu na taarifa sahihi kwa jamii zetu juu ya namna ya kuepuka kwa kufuata kanuni bora za afya pamoja na kuwatumia vyema wahudumu afya za jamii kuanzia ngazi za kijiji na mtaa.
Na hayo yote sasa serikali inataka yakafanywe na wahudumu wa afya wa jamii ambao baada ya tathmini mpya kufanyika wataongezwa kwa baadhi ya vijiji ambavyo ni vikubwa na pia watapatiwa mafunzo maalumu namna ya kukabiliana kutoa elimu sahihi kwa wananchi kuhusu magonjwa Haya.
“Pia Wahudumu wa afya ya jamii hawa waende wakahamashishe jamii zetu kujenga desturi ya kutafuta huduma rasmi za afya ikiwa ni pamoja na kujiunga kwenye mifuko yetu ya bima za afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya,” alisisitiza.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Miradi ya USAID Tulonge Afya Bw Waziri Nyoni ameipongeza serikali kwa maamuzi ya kuufanya mfumo huu wa wahudumu wa afya wa jamii kwa kuufanya uwe rasmi tofauti na awali ambapo kila mdau alikuwa akitumia mfumo wake hivyo kuwa na changamoto nyingi.
Alisema kuwa USAID Tulonge Afya imekuwa ikitumia mfumo wa wahudumu wa afya ya jamii kufanikisha miradi yake mingi ya afya hapa nchini.
Kwa mfano hadi sasa kuna takribani watoa huduma wa afya ya jamii 2200 waliopo katika mikoa 12 na wilaya 29 huku wakitoa baadhi ya huduma wanazozitoa ikiwa ni pamoja na uhamasishaji masuala ya Afya kama malaria, Afya ya mama na mtoto, ukimwi, kifua kijua, na mengine mengi.
Naye Mkurugenzi wa Utafiti, tathmini na Ufuatiliaji, FHI360, Dr Joseph Msofe alisema kuwa kupitia mradi wa USAID Tulonge Afya, wameshirikiana na wizara kuandaa mfumo wa upokeaji na utoaji wa taarifa ambao umeunganishwa katika mfumo rasmi wa Wizara yaani DHIS2.
Kutokana na hili, watoa huduma za afya ngazi ya Jamii au mdau yoyote atakua anafanya shughuli za uhamasishaji jamii ina maana atatakiwa kufuata mfumo na utaratibi huu mzuri na taarifa zote zitaonekana katika ngazi ya wilaya hadi taifa na hivyo kuwawezesha watendaji na watoa maamuzi kujua ni nani anafanya nini na wapi na hivyo kusaidia katika kufanya maamuzi sahihi..
Lakini pia mfumo huu wa ufuatiliaji na utoaji taarifa utasaidia watendaji ngazi zote katika masuala ya afya kuufanya ufuatiliaji ili kubaini penye mapungufu hivyo kuongeza kufahamu maeneo ambayo ufanisi.