……………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi ya kimaendeleo inayoendelea ndani ya Tarafa ya Mihambwe.
Gavana Shilatu aliyabainisha hayo wakati alipofanya ziara ya siku 2 ya kutembelea miradi inayojengwa na kukuta ujenzi ukiwa unashika kasi na mengine ikiwa hatua za mwisho za umaliziaji, kasi ambayo inatoa dira nzuri ya kumalizika kwa wakati.
“Kote nilipotembelea nimejionea kasi ya ujenzi wa miradi ikiendelea. Rai yangu kasi hii iendane na ubora na viwango kulingana na thamani ya fedha. Penye kusifia, nimewapongeza na pale walipoteleza kidogo nimewapa maelekezo warekebishe kasoro kwani Serikali hatutalipokea jengo lenye kasoro na sitarajii hayo.” Alisema Gavana Shilatu wakati akizungumza na Mwandishi wetu juu ya ziara yake.
Katika ziara hiyo, Gavana Shilatu alitembelea ujenzi wa miradi ya kimaendeleo inayoendelea ya Madarasa, Zahanati, Vyoo, Maabara na nyumba ya Mwalimu.
Gavana Shilatu ataendelea na ziara hiyo ya ufuatiliaji ujenzi wa miradi ya kimaendeleo inayoendelea ndani ya Tarafa ya Mihambwe wiki ijayo kujionea ukamilishwaji wa miradi hiyo pamoja na uwekaji wa Madawati kwenye Madarasa mapya yaliyojengwa tayari kwa matumizi.