Sehemu ya Kiwanda (Kinu) cha Mzee Kisangani cha Kuyeyushia Madini ya Chuma kabla ya kupelekwa Kiwandani kwa ajili ya kutengeneza zana za Kilimo.
Baadhi ya Wataalam wakiwa juu ya “Kinu” walikopatiwa maelezo na Mzee Kisangani (wa mwisho) kuona namna kinavyofanya kazi. Wa kwanza ni DKt. Yohana Mtoni (NDC), Prof. Sylivester Mpanduji (SIDO), Prof. Madundo Mtambo (TIRDO) na Leo Mavuka (TAMISEMI).
Timu ya Wataalamu wakipitia kwa pamoja taarifa ya ripoti kwenye ofisi za Tume ya Madini mkoani Njombe, kabla ya kuiwasilisha kwa Waziri wa Madini Doto Biteko.
Mzee Kisangani akiwa Kiwandani kwake anakotengenezea zana mbalimbali zinazotumika Mashambani.
***********************************
Na Issa Mtuwa – Njombe
Timu iliyoundwa na Waziri wa Madini Doto Biteko imekamilisha maagizo iliyopewa baada ya kuwasili Mkoani Njombe kwa Mzee Kisangani.
Maagizo hayo ni pamoja na kuangalia changamoto za jumla zinazomkabili Mjasiriamali huyo katika utekelezaji wa majukumu yake ya Kijasiriamali. Changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa upatikanaji wa Nishati ya
Makaa ya Mawe ya kuyeyushia madini ya chuma, Mtaji wa kuendeshea kiwanda, ukosefu wa leseni za kuchimbia madini ya chuma, eneo la kiwanda cha kutengenezea zana za Kilimo na eneo la kuyeyushia Madini ya chuma, miundombinu mbalimbali.
Akizungumza jana, Aprili 13, 2020 mkoani Njombe, mara baada ya kukamilisha kazi hiyo, Mwenyekiti wa timu hiyo, Prof. Sylivester Mpanduji alisema, timu yake imekamilisha shuguli zote kwa mujibu wa hadidu za rejea walizopewa.
Ameongeza kuwa, timu yake imefurahishwa na shuguli za Mzee Kisangani. Alisema, licha ya kwamba Kisangani hajasoma hata darasa moja na hana Teknolojia ya kisasa lakini amebuni na kutengeneza umeme wa kuendeshea kiwanda chake, kutengeneza kinu cha kuyeyushia madini ya chuma na kuunda kiwanda cha kutengenezea zana zinazotumika mashambani kama vile, Fyekeo, Mapanga, Reki, Visu,Shoka.
Mmoja wa wataalam, kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshugulikia masuala ya Uchumi na Miradi, Leo Mavuka alisema, ipo sababu ya Serikali kuwaongezea nguvu watu wenye ubunifu ili kuinua uwezo wao na kupanua maarifa waliyonayo ili ubunifu
wao usaidie jamii inayo wazunguka kama anavyofanya Mzee Kisangani.
Akizungumzia historia yake, Mzee Kisangani alisema kazi ya Uhunzi alianza mwaka 1991 akiishi na marehemu kaka yake Vicent Mtitu ambae pia alikuwa Muhunzi.
Mwaka 1996 alianza shuguli zake rasmi kwa kujitegemea kazi za Uhunzi. Tangu awali waliendelea kufanya kazi zao bila teknolojia ya kisasa. Walitengeneza zana mbalimbali kwa kutumia teknolojia ndogo kwa kutumia ubunifu.
Amesema, tangu afike Waziri wa Madini Doto Biteko Machi 13-16 mwaka huu mkoani Njombe, baadhi ya changamoto zimeanza kutatuliwa hususani upatikanaji wa Nishati ya Makaa ya Mawe, ujio wa Kamati ya kuangalia shuguli zake na upatikanaji wa leseni za uchimbaji wa madini ya chuma.