Home Siasa MBUNGE WA CHADEMA  AAGA RASMI KUTORUDI BUNGENI 2021

MBUNGE WA CHADEMA  AAGA RASMI KUTORUDI BUNGENI 2021

0
…………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna, Dodoma        
Mbunge wa Bukoba Mjini  Wilfred Lwakatare (CHADEMA) ameaga rasmi bungeni kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu hatagombea tena ubunge na ameamua kupumzike siasa.
Lwakatare ametoa kauli hiyo leo  bunge wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi katika Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ambapo ametaja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake akijivunia kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania.
Mhe.Lwakatare amesema katika utumishi wake alianzia kufanya kazi TAMISEMI kabla ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa mtaa nafasi iliyompa jeuri ya kugombea ubunge akiwa upinzani katika chama cha CUF ambapo alishinda.
Aidha Lwakatare amesema kwenye maisha yake ya ubunge anajivunia mambo mengi ikiwemo ushirikiano mkubwa aliokuwa anapewa na madiwani wa vyama vyote katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba pamoja na watumishi wote.
“Najivunia sana kuwa upinzani na kuimarisha upinzani katika kipindi chote nilichokuwa mbunge na ndani ya upinzani, naondoka nikiwa na furaha na amani nikiomba mbunge atakayekuja baada yangu aendeleze mafanikio haya,” amesisitiza Lwakatare.
Ikumbukwe kuwa Mbunge Lwakatare anakuwa mbunge wa tatu kuaga  kuwa hatagombea katika mkutano huu unaoendelea jijini Dodoma akitanguliwa na Mbunge wa Muleba Kusini Profesa Anna Tibaijuka (CCM) pamoja na Mbunge Abdallah Bulembo (CCM)