……………………………………………………………………..
Joctan Agustino,MAKAMBAKO
Tatizo la kukatika kwa maji kwa baadhi ya maeneo ya mji wa kibiashara Makambako mkoani Njombe limewaibua wafanyabiashara mjini humo ambao wametoa rai kwa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira MAKUWASA kuhakikisha huduma hiyo inapatikana muda wote katika maeneo ya biashara ili waweze kukabiliana na changamoto ya ugonjwa tishio wa CORONA.
Wakizungumzia adha hiyo wafanyabiashara akiwemo Ditrick Komba,Agnes Mbilinyi na Nurdini Matandala wanasema mji huo ambao umekuwa ukikabiliwa na maji ya mgao ni vyema katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya CORONA MAKUWASA ikafanya kila jitihada ya maji muda wote hususani katika mitaa na maeneo yenye misongamano ya watu likiwemo eneo la soko na minada.
Katika hatua nyingine wafanyabiashara hao wametoa ombi kwa mamlaka kuto kata maji kwa kaya ama watumia maji ambao wameshindwa kulipa bili za maji kwa wakati kwani kufanya hivyo kutakwamisha jitihada za mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Naye mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa njombe Siphael Msigala amesema kwa hali ilivyo sasa kuna umhimu serikali kuona namna ya kuwasaidia zaidi wananchi kupata huduma hiyo muda wote kwani mji huo unamwingiliano mkuwa wa watu kutokana na shughuli za kibiashara.
Hata hivyo mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira makambako mhandisi Lufyagile Oscar anasema wanahakikisha maji yanapatikana muda wote hasa katika maeneo ya soko na mikusanyiko ikiwemo Minada na kuwahimiza wananchi kutekeleza jukumu lao la kulipa bili ili kuijengea uwezo wa kujiendesha mamlaka.