Na.Alex Sonna,Dodoma
Serikali imesema kuwa kwa sasa inatoa huduma ya upatikanaji wa vitabu vyote kuanzia shule za msingi na sekondari kwenye maktaba bila malipo yeyote kwa njia ya mtandao.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Joyce Ndalichako wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2020/2021
“Tunajua kuwa wanafunzi kwa sasa wapo nyumbani na wanahitaji kuendelea kupata elimu hata wakiwa nyumbani, tunayohuduma ya maktaba inayotolewa na Taasisi ya Elimu Tanzania ambayo kiutaratibu ili uweze kupata vitabu ilipaswa mtu kulipa, sasa serikali inatoa huduma ya upatikanaji wa vitabu vyote kuanzia shule za msingi na sekondari bila malipo yeyote,”alisema.
Aidha Prof.Ndalichako amewataka wanafunzi kutumia muda wao kusoma vitabu ambavyo serikali imewapa fursa bila gharama yeyote badala ya kuzurura mitaani na kujiweka kwenye hatari ya kupata maambukizi ya Corona.