Home Mchanganyiko TAASISI YA TULIA TRUST YATOA MKOPO WA BAJAJI ZA MILION 120 MBEYA

TAASISI YA TULIA TRUST YATOA MKOPO WA BAJAJI ZA MILION 120 MBEYA

0

Taasisi ya Tulia Trust imekiwezesha Chama cha Bajaj Jiji la Mbeya mkopo wa Bajaj mpya kumi na sita zenye thamani ya shilingi milioni mia moja ishirini ili ziweze kuwasaidia katika kujikimu kiuchumi.
Akikabidhi Bajaj hizo kwenye makao makuu ya ofisi hizo zilizopo Block T Kata ya Iyela Jijini Mbeya Meneja wa Tulia Trust Jacquline Boaz alisema lengo la Taasisi yake ni kuhakikisha vijana wanajiajiri pia kumiliki vyombo vyao badala ya kutegemea waajiri ambao hudai malipo yenye riba kubwa pindi vijana wanapokwama kurejesha kutokomea kusikojulikana na kuzitelekeza familia zao.


Hata hivyo alisema umoja na mshikamano walio nao vijana hao umeiondolea shaka Taasisi yake hata kufikia kudhamini mkopo huo mkubwa.
“Taasisi yetu imekuwa ikishirikiana na makundi ya vijana wa Bodaboda,Bajaj na Wafanyabiashara ndogo ndogo ili kuwaondolea usumbufu na urasimu wa mikopo kutoka Taasisi za kifedha” alisema Jacqueline.
Kwa upande wake mratibu wa miradi wa Taasisi ya Tulia Trust Joshua Mwakanolo alisema vijana hao wa Bajaj wakirejesha kwa wakati mkopo huo utatoa fursa kwa wengine nao kukopeshwa Bajaj.


Akipokea Bajaj hizo kumi na sita Mwenyekiti wa Bajaj Jiji la Mbeya Iddi Ramadhan aliishukuru Taasisi ya Tulia Trust kufanikisha mkopo huo ambao umewapa hamasa ya maendeleo vijana na kwamba kupitia mkopo huo Bajaj hizo zimeongeza ajira lakini pia serikali itapata kodi hivyo kuongeza pato la Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Naye Katibu wa waendesha Bajaj Jiji la Mbeya Dickson Kiswaga alisema Taasisi ya Tulia Trust inayoongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetimiza ndoto yao ya kumiliki Bajaj zao kwani kabla ya kufanikiwa mkopo huo waliomba maeneo mbalimbali bila mafanikio hivyo alitoa wito kwa wanufaika wa mkopo huo kulipa kwa wakati ili wenzao nao wakopeshwe.


Maria Mbawa mwanamke pekee aliyenufaika na mkopo huo hakusita kuishukuru Taasisi ya Tulia Trust kuwasaidia wanyonge na mwanamke kama yeye ingekuwa ndoto kwake kumiliki Bajaj ambapo aliahidi kuitunza pia kurejesha mkopo kwa wakati.
Festo Stephen Mwandemwa,Meshack Mwakaselema,Yusuph Mwagawa, Venance Mwakihaba,Patrick Mwansasu na Clinton Mwakabungu kwa niaba ya wenzao waliopewa mkopo wa Bajaj mbali ya kuishukuru Taasisi hiyo kwa kuwapatia mkopo pia wamepata ajira hivyo wameahidi kurejesha kwa wakati ili wengine nao waweze kunufaika.


Bajaj hizo aina ya TVS zilipendekezwa na Chama hicho cha waendesha Bajaj hivyo vijana hao wanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika Jiji kwa kumiliki Bajaj zao.
Asilimia ishirini za Bajaj zimetolewa na Taasisi ya Tulia Trust na asilimia themanini zimetolewa na Benki ya CRDB.
Mbali ya kukabidhi mkopo wa Bajaj Taasisi ya Tulia Trust imekabidhi sare za usalama barabarani ili waendesha Bajaj waweze kuonekana hasa nyakati za usiku.
Hivi karibuni Jiji la Mbeya lilitoa mkopo wa pikipiki kwa kikundi cha Bodaboda SAE Jijini Mbeya ambacho mlezi wake ni Dkt Tulia Ackson