Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma,Bw. Godwin Kunambi akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake leo jijini Dodoma kuhusiana na uzinduzi wa Stendi kuu ya Mabasi, Soko kuu la Ndugai na kituo cha mapumziko cha Chinangali Park yanayotarajia kuzinduliwa rasmi April 26 mwaka huu.
……………………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Wakazi wa Dodoma pamoja na maeneo ya jirani wametakiwa kuchangamkia fursa ya kuchukua fomu kwajili ya kupata maeneo ya kuwekeza biashara mbalimbali katika miradi ya kimkakati ya Stendi kuu ya mabasi, Soko kuu la Ndugai na kituo cha mapumziko cha Chinangali Park kinachotarajia kuzinduliwa rasmi April 26 mwaka huu jijini Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw.Godwin Kunambi, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake leo kuhusu mkakati wa jiji hilo walivyojipanga kuzindua miradi mbalimbali.
Kunambi, ameeleza kuwa miradi hiyo mitatu ya kimkakati yote tayari imeshakamilika kwa asilimia 100.
“Hivyo natoa wito kwa wakazi wa Dodoma na maeneo mengine nchini kuzitumia fursa zinazotokana na miradi hii mikubwa ya kimkakati katika kuleta maendeleo ya nchi na kukuza uchumi wa taifa letu”, ametoa wito Kunambi.
Kunambi amesema kuwa mradi wa stendi kuu ya mabasi ya mikoani itakuwa na uwezo wa kuchukua watu 1,200 kwa wakati mmoja wanaosubiria usafiri.
“Stendi hii itakuwa ni ya kimataifa Afrika mashariki itakuwa ya kwanza stendi ambayo ina eneo la watu maalum (VIP) na imejengwa kwa kisasa na kwa hili sisi wana Dodoma tunamshukuru sana Rais Magufuli”ameeleza Kunambi
Aidha Kunambi ameongezea kuwa ujenzi wa soko kuu la Ndugai litahudumia kata zote 41, za jiji la Dodoma.
Katika kituo cha kupumzikia cha Chinangali Park, amesema kuwa kitakuwa na michezo mbalimbali ikiwemo kuongelea, Tenes na michezo mbalimbali pamoja na vyakula na vinywaji.
Kunambi amesema kuwa Miradi hiyo ya kimkakati iliyogharibu zaidi ya Sh. Bilioni 89 inatarajia kuzinduliwa rasmi Aprili 26 mwaka huu hivyo wakazi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla wakae mkao wa kula ili kutumia fursa hizo kuzalisha na kuongeza kipato chao.
Aidha amesema kuwa jiji linatarajia kukamilisha ujenzi wa kituo cha malori ambacho kitakuwa na uwezo wa kuegesha malori 300, kwa wakati mmoja.