****************************
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu na ajali za barabarani ili kuhakikisha kuwa wageni na wakazi wa Mkoa huu wanaendelea kuwa salama na mali zao.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa usalama hali inayopelekea kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu
pamoja na ajali za barabarani.
KUJIPATIA MALI KWA NJIA YA UDANGANYIFU.
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watuhumiwa wanne 1. ENOCK KYARUZI [41] Mkazi wa Dar es Salaam 2. SATALA MAKOBA [50] Mkazi wa Dar es Salaam 3. MICHAEL CHUWA [65] Mkazi wa Dar es Salaam na 4. DICKSON JUMA WARIOBA [34] Mkazi wa Mlowo Mkoa wa Songwe kwa
tuhuma za kujipatia mali mbalimbali zenye thamani ya Tshs.19,680,000/= zikiwemo Televisheni 13 za inchi mbalimbali kwa njia ya udanganyifu.
Watuhumiwa walikamatwa tarehe 03.04.2020 huko Jijini Dar es Salaam katika maeneo tofauti baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kupata taarifa na kufanya msako
na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa pamoja na mali hizo.
Ni kwamba watuhumiwa walijipatia mali hizo baada ya kufanya udanganyifu kwa mfanyabiashara aitwaye MICHAEL MDOPE anayemiliki duka lililopo SIDO Jijini
Mbeya la vifaa vya muziki na Televisheni na kisha kutoa “order” ya kutaka kununua Televisheni za ukubwa tofauti 24 na kuomba malipo yafanyike kwa njia ya hundi wakati wakijua hundi hiyo ni hewa.
Baada ya tukio hilo na taarifa kuripotiwa Polisi upelelezi ulifanyika na kubaini kuwa watuhumiwa walifanya udanganyifu katika kujipatia mali hizo kwa kutumia hundi
hewa. Watuhumiwa wamekutwa na Televisheni kumi na tatu [13], Homebase inchi 65 moja, Aborder inchi 55 moja, Aborder inchi 43 mbili, LG inchi 43 moja na Aborder inchi 32 saba, Home Theater aina ya Sony na Gari namba T.681 DGV Toyota Brevis ambalo walilitumia kusafirishia mzigo huo.
Hili ni tukio la pili kutokea ndani ya wiki moja kwani tarehe 24/03/2020 alikamatwa mtuhumiwa ADELHARD METHOD @ MGENI [37] Mfanyabiashara na Mkazi wa Njombe kwa tuhuma za kujipatia mali zenye thamani ya Tshs.9,660,000/= kwa njia ya udanganyifu toka dukani kwa Mfanyabiashara aitwaye BENEDICTO MBILINYI
[55] Mkazi wa Block “T”. Upelelezi wa shauri hili unaendelea.