Home Siasa PROF.TIBAIJUKA AAGA BUNGENI KWA MACHOZI YA SAKATA LA ESCROW

PROF.TIBAIJUKA AAGA BUNGENI KWA MACHOZI YA SAKATA LA ESCROW

0

MBUNGE wa Muleba Kusini mkoani Kagera Profesa Anna Tibaijuka ametangaza rasmi kuwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu wa 2020 hatagombea tena nafasi ya ubunge na anakwenda kupumzika
huku akitumia nafasi hiyo kuelezea namna alivyoumizwa na sakata la fedha za Escrow.

Profesa Tibaijuka ametangaza uamuzi wake wa kutogombea tena ubunge kwenye jimbo hilo leo Aprili 3 mwaka 2020 ambapo ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa wananchi wa Muleba kwa namna ambavyo wamempa ushirikiano katika kipindi chote cha miaka 10 ambacho amekwa mbunge wao na anaondoka kwenye nafasi hiyo akiwa imara na mwenye kukubalika jimboni.

“Mheshimiwa Spika wa Bunge , kwanza nakushukuru wewe kwa kuliongoza Bunge letu vizuri, natoa shukrani zangu kwa Waziri Mkuu kutokana na hotuba yake nzuri, natoa shukrani kwa Rais wetu  Dk.John Magufuli kwa kazi ambayo ameifanya ya kuleta maendeleo.Hata hivyo naomba nieleze katika uchaguzi mkuu mwaka huu sitagombea tena ubunge, nakwenda kupumzika,”amesema Profesa
Tibaijuka.

Hata hivyo ametumia nafasi hiyo kuelezea kuwa wakati anatangaza kuaga Bungeni ni vema akaweka rekodi sawa.”Baada ya sakata la Escrow ambalo nami nilituhumiwa nilikosa kabisa nafasi ya kujitetea ndani ya Bunge maana sikupewa nafasi.Hivyo niliamua kuwasilisha hoja binafsi na wakati ule wa Spika akiwa Anna Makinda haikupata nafasi ya kupokelewa.

“Nashukuru sasa hoja yangu binafsi Spika Job Ndugai amekubali kuipokea na kuikabidhi kwa Serikali.Kuna mambo ambayo nimejifunza nikiwa bungeni na nikitoka hapa nakwenda kuandika vitabu kuzungumzia haya ambayo nimeyaona na kujifunza bungeni,”amesema Profesa Tibaijuka na kuongeza kuna haja ya  kuboresha demokrasia ndani ya Bunge.

Baada ya Profesa Tibaijuka kutangaza kung’atuka kwenye nafasi hiyo, Spika Ndugai ametumia nafasi hiyo kumpongeza kwa uamuzi wake huo na kuwataka wabunge wote kumpongeza kwa kumpigia makofi
mengi.”Umetoa hotuba nzuri sana na iliyojaa busara, tunapongeza kwa uamuzi wako.”