****************************
Dar es Salaam, Machi 24, 2020. Hivi karibuni, Watanzania wengi wameungana na dunia nzima katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 (maarufu Corona).
Katika miezi na wiki zijazo juhudi za pamoja zinahitajika ili kusaidiana na serikali katika kupambana na athari za mlipuko wa ugonjwa huu.
Jihitada za kuisaidia jamii kutatua changamoto mbalimbali kama ilivyo kwa janga hili la COVID-19 ni mojawapo ya majukumu ya Vodacom Tanzania PLC katika kusaidia jamii na wadau wake. Kipaumbele cha Vodacom ni afya na usalama wa wafanyakazi wake zaidi ya 560, na wakati huo huo kuendelea kutoa huduma, kuunganisha na kusaidia wateja wake kwa kuzingatia miongozo ya serikali na wizara zake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Hisham Hendi anasema, Vodacom ina majukumu muhimu katika kipindi hiki kisicho cha kawaida. Tuna mkakati wa kuhakikisha kuwa biashara yetu inakuwa endelevu wakati wote. Niwahakikishie Watanzania kuwa wataendelea kupata huduma zetu kwa kuunganishwa na marafiki na familia na kwamba biashara itaendelea kufanyika kwa kutumia njia za kidijitali kupitia mtandao wetu ulioboreshwa.
Hendi aliongeza kuwa, “Wakati huo huo tunaweka juhudi za pamoja, kuwasaidia wanafunzi ambao kwa sasa wamefunga shule ili waweze kupata nyenzo za kujisomea kwa njia ya kidijitali kwa kutumia mitaala inayokubalika kimataifa.
Kupitia mfumo uliopitishwa kimataifa wa Khan Academy http://instantschools.vodacom.co.tz/user/#/signin wanafunzi ambao wako nyumbani kutokana na janga hili wanaweza kuendelea kujisomea ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua stahiki za kujikinga na ugonjwa wa COVID-19.
Vodacom imechukua hatua kadhaa kusaidia jamii kupambana na mlipuko wa COVID-19, hatua hizi ni pamoja na:
Tumeweka mpango thabiti wa kuhakikisha kunakuwa na mwendelezo wa biashara kuanzia ngazi ya kanda, Taifa na kimataifa, lakini pia mpango wa kuwahudumia wateja kwa kutoa majibu sahihi juu ya maswasli yao, pale wanapohitaji ufafanuzi wa huduma zetu mbalimbali.
Tumeongeza uwezo wa wafanyakazi wetu kufanya kazi wakiwa mbali kama vile majumbani bila tatizo lolote.
Tumetoa ushauri wa kina kwa wafanyakazi wetu. Tuna mfumo sahihi wa usafi katika ofisi zetu na maduka yetu yote nchi nzima.
Tumeunda kikosi maalum cha COVID-19 kwa ajili ya kuhakikisha huduma zote zinatolewa kwa wateja wetu kwa usahihi. Tuna huduma mbalimbali za kidijitali kwa ajili ya wateja wetu. Huduma zetu za kila siku zitaendelea kama kawaida kwa ubora zaidi na bila kikwazo chochote.
Huduma za data, sauti na kuunganishwa tunazotoa zitamuwezesha mteja kupata huduma wakati wote huku akipunguza hali ya mgusano na msongamano. Mtandao wetu una uwezo wa kutosha kuwawezesha wateja wetu na wafanyabiashara kufanya kazi kwa tija zaidi.
Mawasiliano ni nyenzo muhimu katika sekta zote, upatikanaji wa mawasiliano ni kiungo muhimu katika kuunganisha sekta zote kiuchumi .
Hadi sasa hatujapata usumbufu wowote katika utoaji wa huduma zetu. Tuna utaratibu maalumu katika hatua za awali wa kuzuia usumbufu na tunafanya kazi kwa karibu na watoa huduma wetu na wadau wengine.
Vodacom inatoa fursa ya kupata taarifa za COVID-19 bila malipo kupitia katika tovuti mbalimbali za serikali. Hii ina maana kwamba mtumiaji wa Vodacom anaweza kupata taarifa za msingi katika tovuti hizo ambazo ni pamoja na: http://www.mcdgc.go.tz/ (Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto ), https://www.habari.go.tz/(Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ) http://www.maelezo.go.tz/(Idara ya Habari Maelezo) Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, tunatoa huduma ya ujumbe mfupi (SMS) kwa zaidi ya wateja wetu milioni 14 nchi nzima juu ya usafi na taarifa nyingine zinazohusu ugonjwa huu.
Tumesaidia huduma ya intaneti kwa kitengo maalum cha serikali kinachoshughulikia mlipuko wa COVID-19 katika maeneo mbalimbali na kuwawezesha kuwa na mawasiliano wakati wote.
Kutoa huduma ya kusaidia mfumo wa elimu kwa kipindi hiki ambacho wanafunzi wako majumbani. Watumiaji wa Vodacom na wasiokuwa watumiaji wanaweza kupata huduma ya Shule Papo Hapo (Vodacom Instant Schools) bila malipo yoyote; Hili ni jukwaa huru kwa wote ambapo watumiaji wa Vodacom wanaweza kupata masomo mbalimbali kwa kuzingatia mitaala ya shule za msingi na sekondari. Maudhui yake yanahusisha masomo, majaribio, chemsha bongo na video za masomo ambazo zinalenga kuwasaidia wanafunzi ambao kwa sasa wako majumbani.
Huduma hii inapatikana kupitia simu ya mkononi, kompyuta mpakato, Vishikwambi na kompyuta za kawaida.
Wanafunzi wanaotumia portal ya Instant Schools wanaweza kufanya mazoezi na kudurusu masomo ambayo walishayafanya wakiwa shule. Lakini pia kutafuta mitihani ya nyuma, na kupata dondoo za namna ya kuongeza kiwango chao cha ufaulu, kupata masomo mbalimbali na kuangalia video zake.
‘Tunasisitiza utayari wetu na kuendelea kujitolea kusaidia juhudi za serikali, na kufanya kila tuwezalo hadi mwisho. Tutaendelea kuzungumza na serikali ili kupata njia mbadala zaidi kufanikisha juhudi zetu. Mafanikio katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu yatategemea nguvu ya pamoja kutoka kwa kila raia katika kuchukua jukumu la kuzuia kuenea kwa janga hili. Sote tunatakiwa kushiriki kwa pamoja katika kupambana na janga hili. Kwa hivyo tunawasihi watanzania kufuata ushauri wa serikali na huduma za afya na wajitunze na familia zao Hendi alimalizia kusema.
Kuhusu Vodacom: Vodacom Tanzania PLC ni watoa huduma ya mawasiliano ya simu za mkononi wanaoongoza wenye mtandao wa data wenye kasi zaidi nchini. Tunatoa huduma za mawsiliano kwa zaidi ya wateja milioni 14.
Kampuni ya Vodacom Tanzania pamoja na kampuni zake tanzu ni sehemu ya Kundi la makampuni ya Vodacom (Vodacom Group) iliyosajiliwa Afrika Kusini ambayo kwa upande mwingine inamilikiwa na kundi la makampuni la Vodacom Plc la Uingereza. Kampuni ya Vodacom imesajiliwa katika Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) kwa namba ISIN: TZ1886102715 Stock name: VODA.