Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na Waandishi wa habari.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akieleza jambo wakati wa kikao na Waandishi wa habari, kilichofanyika Jinjini Dodoma.
Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya Benjamin Mkapa Dkt. Ellen Mkondya akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari, katika Mkutano ulioongozwa na Waziri wa Afya leo Jijini Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akieleza jambo wakati wa kikao na Waandishi wa habari, kilichofanyika Jinjini Dodoma. katikati ni naibu waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula (wakwanza kushoto).
*********************************
Na Rayson Mwaisemba, WAMJW-DOM
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Taasisi ya Benjamini Mkapa inayotekeleza mradi wa Uimarishaji mifumo endelevu na stahimivu ya Afya kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu, imeajiri jumla ya watumishi 307 ikiwa ni muendelezo wa kuimarisha huduma za Afya nchini.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kikao na Waandishi wa habari, kilichofanyika Jinjini Dodoma.
“Tunapenda kuwataarifu mwendelezo wa kazi nzuri inayotekelezwa kupitia mradi huu na kwamba taratibu za ajira kwa wataalam wa afya wengine 307 zimekamilika. Lengo kuu la zoezi hili ni kuongeza nguvu katika utoaji huduma katika sekta ya afya”, alisema Waziri Ummy.
Katika kikao hicho kilichohudhuliwa na Naibu Waziri wa Afya na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula, Waziri Ummy amesema kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Mkapa, kuanzia mwaka 2018 hadi February 2020, imeweza kuajiri jumla ya watumishi wa afya 461 ambao wanatoa huduma za afya sehemu mbalimbali nchini.
Aliendelea kusema kuwa, Watumishi hawa watahudumu kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizopo katika mikoa 12 ya Kagera, Mwanza, Geita, Simiyu, Mara, Shinyanga, Kigoma, Tabora, Katavi, Dodoma, Songwe na Kilimanjaro.
Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa, wataalamu hao 307 wameshapangiwa kufanya kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 68 zilizopo katika Mikoa 11, huku akibainisha kuwa Mikoa iliyonufaika ni Mwanza (34), Shinyanga (33), Mara (43), Simiyu (51), Geita (30), Kagera (34), Katavi (41), Tabora (43), Dodoma (27), Arusha (10) na Kigoma (42).
Alisema kuwa, Kupitia mchakato huu wa ajira, Kada sita za wataalamu wa Afya zimenufaika na kibali hiki kwa mgawanyo ufuatao; Kada ya Wauguzi wenye cheti (59), Wauguzi wenye Diploma (30), Maafisa Tabibu (73), Maafisa Tabibu Wasaidizi (100), Wataalamu wa maabara ngazi ya cheti (25) na ngazi ya Diploma (20).
Mbali na hayo, Waziri Ummy ameendelea kuwahimiza wataalamu wote waliopangiwa maeneo ya kufanyia kazi kuripoti mara moja kuanzia tarehe 23 hadi 27 Machi 2020, na kuanza kutekeleza majukumu yao katika vituo watakavyopangiwa.
“Napenda kuwahimiza wataalamu wote waliopangiwa maeneo ya kufanyia kazi kuripoti mara moja kuanzia tarehe 23 hadi 27 Machi 2020, ili kuanza kutekeleza majukumu yao katika vituo watakavyopangiwa” alisema
Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa, Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa upataji taarifa (mawasiliano), huku akiwataka waombaji kufanya maombi ndani ya muda ulioelekezwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Dkt. Ellen Mkondya amesema kuwa, taasisi ya Benjamin Mkapa kwa miaka 14 imetoa ajira za wataalam wa afya 2181 ambao wamekuwa wakitoa huduma katika Hospitali na Vituo vya tiba nchini kote, hususan vituo vya serikali na baadhi kwenye vituo vya kidini.
“Taasisi ya BMF kwa miaka 14 yote tokea mwaka 2006 hadi Desemba 2019, tumeshaweza kutoa ajira za wataalam wa afya 2181 ambao wamekuwa wakitoa huduma katika Hospitali na Vituo vya tiba nchini kote, hususan vituo vya serikali na baadhi kwenye vituo vya kidini” alisema.