NA DENIS MLOWE, IRINGA
MSANII wa muziki wa bongo fleva anayekuja kwa kasi kutoka Nyanda za Juu Kusini mwenye makazi yake mkoani Iringa, Ezra Msiliova ‘ Eze Nice’ ametoa wito kwa wadau wa muziki huo kuzipokea kwa nguvu zote nyimbo zake mbili anazotarajia kuziachia hivi karibuni.
Akizungumza na Mwanahabari, Eze Nice alisema kuwa nyimbo hizo mbili ni zawadi tosha kwa Rais John Magufuli na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Iringa, Salim Abri ‘Asas’ kwani amezipa majina Magufuri na Asas ikiwa ni vile ambavyo wameweza kufanya makubwa kwa maendeleo ya nchi na mkoa wa Iringa kwa ujumla.
Eze Nice ambaye amejichukulia maarufu mkoani Iringa kwa kuwa na nyimbo mbalimbali za kuhamasisha maendeleo na nyingine nyimbo za siasa amekuwa msanii wa kwanza kutoka mkoani hapa kuweza kuimba wimbo wa kumsifia Magufuli na Salim Abri kwa kuona wanastahili sifa hivyo kutoa zawadi za nyimbo hizo kwao.
Alisema kuwa wimbo huo wa kwanza unajulikana kwa jina la Magufuli ambao ameelezea kwa undani kazi zilifanywa na Rais kwa kipindi hiki na wimbo wa pili ni zawadi kwa Salim Abri ambaye amekuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa mkoa wa Iringa hivyo ili kuwaenzi kwao ametunga nyimbo hizo.
Alisema kuwa nyimbo hizo ambazo zimefanywa chini ya mzalishaji yeye mwenyewe kwenye studio .New Record ya mjini Iringa zinatarajia kuwa kali kwani ziko katika mahadhi ya rumba na nzuri kwa ajili ya kucheza na kusikiliza ujumbe uliotolewa.
“Mwandishi nikwambie kitu hawa watu wamefanya makubwa sana kwa tanzania na mkoa wa wetu Rais wetu kafanya yake Tanzania na kwa upande wa Mnec Salim Asas kwa mkoa wa Iringa kafanya mengi sana kwa kweli hivyo zawadi hii nawapa wao kila mmoja kwa kuwa na wimbo wake,” alisema
Alisema kuwa nyimbo zote zinafanyiwa video na Shama Kilasi ambaye amekuwa akifanya video za wasanii wengi wa Nyanda za Juu Kusini na anatarajia baada ya wiki mbili au tatu zitatoka na watu waweze kuziona ubora wake na ujumbe uliomo kwenye nyimbo hizo.
Aidha alisema kuwa kwa upande wake kwa sasa ataachia wimbo mmoja mmoja hadi pale ambapo jamii itamtambua vyema na kutoa albamu kali ambazo zitaheshimika nchini.
Aidha Eze Nice alivishukuru vyombo vya habari kwa kuweza kumsimamia katika kazi zake zinaonekane kwa kuzipiga au kumtolea habari zake na kutoa wito kwa wasanii wengine kutokata tamaa kwa kuwa Sanaa yoyote inahitaji sana nidhamu, heshima na uvumilivu ili kuweza fikia malengo.
Alisema kuwa malengo yake kuwa msanii mkubwa ambaye ataleta mabadiliko makubwa katika Sanaa ya muziki akiwa chini ya kampuni hiyo kwa kuwa malengo yapo na nia anayo katika kufikisha muziki mbali Zaidi kuliko ilivyo sasa.
Alisema kuwa amejipanga vyema kuweza kukabiliana na changamoto zilizoko katika Sanaa ya muziki wa bongo fleva akiwemo baadhi ya radio kuchagua wasanii na kuacha kucheza nyimbo nzuri za wasanii wanaibuka miaka ya hivi karibuni.