Mbunge wa Jimbo la Ukonga, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwitan Waitara akizungumza wakati wa kukagua maandalizi ya ujenzi wa Daraja la Ulongoni A na ujenzi wa kivuko cha muda cha watembea kwa miguu, Bodaboda na Bajaji katika Jimbo hilo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meya wa Manispaa ya Ilala, Omary Kumbilamoto. Picha na Richard Mwaikenda
Mbunge wa Jimbo la Ukonga, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwita Waitara akimsikiliza kwa makini Pieter Mare wa Kampuni ya UWP Consulting Engineer, wakati Waitara alipokwenda kukagua maandalizi ya ujenzi wa madaraja ya Ulongoni A na B, Ukonga Dar es Salaam.
Baadhi ya wakazi wa Ulongoni wakipita kwa tahadhari kubwa kwenye kidaraja katika eneo linalotrajiwa kujengwa daraja Ulongoni A.
Waitara (Wa pili kushoto), akiondoka baada ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa Daraja la Ulongoni A.
Mbunge wa Jimbo la Ukonga, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwitan Waitara akizungumza katika mkutano na wajenzi wa madaraja ya Ulongoni A na B pamoja na viongozi wa Manispaa wa Ilala.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema akizungumza kabla ya kumkaribisha Mbunge wa Jimbo la Ukonga, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwita Waitara
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri akielezea kuhusu mradi wa ujenzi wa madaraja ya Ulongoni A na B.
Meya wa Manispaa ya Ilala, Omary Kumbilamoto akizungumza katika kikao hicho, kuhusu ujenzi wa miradi hiyo iliyosababisha changamoto kubwa kwa wakazi wa Ulongoni
Baadhi ya wadau wakiwa katika kikao hicho.
****************************************
Na Richard Mwaikenda, Ukonga.
MBUNGE wa Jimbo la Ukonga, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mwita Waitara amewataka wakandarasi wa madaraja ya Ulongoni A na B, kukamilisha ujenzi kwa wakati.
Alitoa maagizo hayo wakati wa kikao cha makabidhiano ya kuanza miradi hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Anatoglou jijini Dar es Salaam jana.
Madaraja hayo yanajengwa upya na kampuni mbili tofauti kwa gharama ya sh. bil. 17, baada ya kuzolewa na mafuriko yaiyosababishwa na mvua kubwa katika Mto Msimbazi.
Kampuni ya Chonqging International Construction Corporation inajenga Daraja la Zimbili/Ulongoni A kwa gharama ya sh. bil. 4 na China Railway Seventh Group inajenga Daraja la Ulongoni B pamoja na kipande cha barabara cha Km 7.5 kwa gharama zaidi ya sh. bil. 17.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, Waitara aliwataka wakandarasi hao kuanza haraka ujenzi huo ili ukamilike mapema na kuwaondolea adha wanayopata wakazi wa Ulongoni ambao kwa asilimia kubwa hutegemea mahitaji yao upande wa pili Gongo la Mboto.
Waitara amekemea tabia ya baadhi ya wananchi kuchelewesha kwa makusudi ujenzi kwa kuwaingilia wakandarasi wanapotekeleza wajibu wao, ambapo aliwataka na ushauri mzuri waupeleke kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.
Baada ya kumalizika kikao hicho, Waitara alifanya ziara ya kukagua maandalizi ya ujenzi wa madaraja hayo, huku akiambatana na Meya wa Manispaa hiyo, Omary Kumbilamoto Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Jumanne Shauri pamoja na Mhandisi Ujenzi wa Mradi wa DMDP, John Magori.
Katika Daraja la Ulongoni B, alikuta ujenzi ukiendelea wa kivuko cha muda cha waendesha bodoboda, bajaji na watembea kwa miguu. Ujenzi wa madaraja ya kudumu aliambiwa utaanza rasmi mapema mwezi ujao mvua za masika zikiisha.