**************************************************************
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Masiliano Tanzania, TTCL limefanikisha Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufanyika kwa njia ya mtandao (Video Conference) kufuatia mlipuko wa ugonjwa hatari wa Corona unaoendelea kuzikumba nchi nyingi Duniania.
Mkutano huo umeanza Machi 16 mwaka huu kwa maofisa waandamizi kutoka nchi 16 wanachama kushiriki vikao wakiwa katika nchi zao, kabla ya kufunguliwa rasmi jana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa jijini Dar es Salaam huku akiwahutubia mawaziri wote wakiwa katika nchi zao.
Mkutano huu wa mawaziri wa SADC pamoja na mambo mengine unajadili hatua zaidi za utekelezaji wa Kauli mbiu ya mwaka huu ya Jumuiya ya SADC inayosema ‘Mazingira wezeshi kwa ajili ya Maendeleo Endelevu na Jumuishi ya Viwanda, Kukuza Biashara na Ajira ndani ya SADC’.
Akizungumza na Wandishi wa Habari mara tu baada ya Mhe. Waziri Mkuu kufungua mkutano huo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema kufanikisha mkutano huo kufanyika kwa mfumo wa ‘video conference’ ni jambo la kujivunia kama nchi kwani limewezesha kukidhi matakwa ya Shirika la Afya Duniani la watu kujihepusha na misongamano ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Amesema TTCL imeandika historia mpya ya kuwezesha mkutano huo kufanyika kisasa zaidi kwani hii ni mara ya kwanza kwa nchi wanachama wa SADC kufanikisha mkutano huo kwa mfumo wa ‘video conference’. “Tanzania imewekwa kwenye kumbukumbu kwani imeweza kufanya mkutano huo kwa njia ya ‘video conference’ hii ikiwa ni mara ya kwanza,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Kindamba.
Amesema hatua hii imefanikiwa ikiwa ni kutii maagizo ya Mwenyekiti wa SADC Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli baada ya Mawaziri wa Afya wa SADC kukutana kwa kikao cha dharura jijini Dar es Salaam na kushauri vikao vyote vya jumuiya hiyo vifanyike kwa njia ya mtandao mpaka hapo ugonjwa wa Corona utakapodhibitiwa.
“Tumewezesha na tumelifanikisha kwa vitendo suala hili hivyo niwapongeze sana wahandisi wa TTCL na Wizara husika pamoja na wadau wote kwakuhakikisha jambo hili linawezekana bila mkwamo wowote,” Alisema Kindamba.
Aidha aliongeza kuwa TTCL imeweza kuunga mkono juhudi za serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kutoa mchango wake wa huduma hiyo ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona, ambapo ushauri wa wizara hiyo ilikuwa kupunguza mkusanyiko wa wananchi kujiepusha na maambukizi ya corona.
Hata hivyo, Waziri Kindamba amewatoa wasiwasi taasisi, mashirika ya umma na binafsi kuwa TTCL inatoa huduma hii kuwezesha mikutano, semina, warsha na elimu mtandao kwa watakaohitaji huduma hiyo ili kufanikisha majukumu hayo hasa katika kipindi hiki ambacho Dunia iko kwenye mapambano ya ugonjwa wa corona na kuzuia msongamano.
Kindamba amebainisha kuwa mpaka sasa zipo taasisi zaidi ya sita amabazo zimeomba huduma hii ili kuwa sehemu ya mapambano ya corona. TTCL kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imeweka namba maalum kwa ajili ya mtu kupiga simu bure kutoa taarifa za mgojwa wa Corona au kujipatia taarifa mbalimbali kuhusu ugonjwa huu.
“…sisi na Wizara ya Afya tumeweka timu moja kwa ajili ya kituo cha miito (call center) ili kuwahudumia wananchi saa ishirini na nne waweze kutoa taarifa za mtu mwenye dalili za ugonjwa wa corona au kujipatia taarifa mbalimbali kuhusu ugonjwa huu,” alisema Kindamba.